BURUNDI-MACHAFUKO

Mauaji mwishoni mwa wiki hii katika baadhi ya maeneo ya Bujumbura

Mtu huyu akibeba jeneza kwenye baiskeli yake tarafani Kanyosha, moja ya vitongoji vya mji wa Bujumbura, Januari 10, 2016.
Mtu huyu akibeba jeneza kwenye baiskeli yake tarafani Kanyosha, moja ya vitongoji vya mji wa Bujumbura, Januari 10, 2016. © GRIFF TAPPER / AFP

Mwishoni mwa wiki hii, milio ya risasi na milipuko ya maguruneti ilisikika katika maeneo ambayo ni kitovu cha maandamano dhidi ya muhula watatu wa rais Pierre Nkurunziza.

Matangazo ya kibiashara

Watu wasiopungua watatu waliuawa, askari polisi wawili walijeruhiwa na watu watano walikamatwa. Miongoni mwa waathirika wa Jumamosi Januari 9, ni pamoja na kijana mmoja mpiga picha aliyeuawa na polisi. Mazingira ya kifo chake yametatanisha, Jumapili hii jioni.

Alfred Baramburiye alikuwa mpiga picha tarafani Nyakabiga. Alikuwa akirudi nyumbani siku ya Jumamosi baada ya kumaliza kazi yake ya kupiga picha wakati alipokutana na askari polisi wakipiga doria. Kwa mujibu wa mashahidi waliowasiliana na RFI, aliposhuka gari, Alfred Baramburiye aliwasabahi askari polisi waliokuwa eneo hilo. Bila kuchelewa askari polisi hao walimkamata na kuanza kumshtumu kwamba anahusika na mashambulizi ya mabomu yaliowaua askari polisi hivi karibuni tarafani Nyakabiga. Kijana huyo alipiga kelele akiomba msaada, lakini muda mfupi baadaye alikutwa ameuawa.

Msemaji wa polisi amekanusha madai hayo. Pierre Nkurukiye amesema kijana huyo hakukamatwa na askari polisi, lakini aliuawa katika mapigano kati ya vikosi vya usalama na wahalifu. Mtu mwingine alipigwa risasi tarafani Musaga na vikosi vya usalama ambavyo vilimjeruhi mtu mwengine tarafani humo Jumapili hii asubuhi.

Mtu wa tatu aliuawa katika kata ya Jabe, tarafani Bwiza ambapo maguruneti matatu yalirushwa Jumamosi, kwa mujibu wa msemaji wa polisi. Tarafani Nyakabiga, guruneti nyingine iliwajeruhiwa askari polisi wawaili ikiwa ni pamoja na mmoja ambaye alijeruhiwa vikalii. Tarafa za Ngagara na Cibitoke pia zilishuhudia ghasia kama hizo mwishoni mwa wiki hii. Kwa kujitetea, polisi imedai kuwa imewakamata watu watano, bunduki tano na maguruneti mawili.