BURUNDI-UN-MACHAFUKO

UN ina hofu ya kutokea kwa janga kubwa la mauaji Burundi

Askari polisi wa usalama wa rais wakipiga doria wilayani Ngagara, jijini  Bujumbura, Aprili 27, 2015.
Askari polisi wa usalama wa rais wakipiga doria wilayani Ngagara, jijini Bujumbura, Aprili 27, 2015. AFP PHOTO / SIMON MAINA

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipokea tarehe 6 Januari, waraka uliyoandikwa na mkuu wa Operesheni za Kulinda Amani Hervé Ladsous.

Matangazo ya kibiashara

Waraka huo unazungumzia hali ya kisiasa, uchumi na kijamii ambayo ni tete nchini Burundi, na kubaini uwezekano wakutokea matukio matatu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kimbari. Kama mauaji ya kimbari yatatokea, Umoja wa Mataifa haujakua tayari kuchukua hatua zinazohitajika kwa kuzuia mauaji hayo, Ladsous aliandika.

Waraka huu ulikua ni siri na ulikua unalenga kukidhi mahitaji ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kuandaa mpango wa kupeleka askari nchini Burundi iwapo machafuko yataongezeka. Lakini waraka uliotumwa na Hervé Ladsous kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unaenda mbali zaidi na unaelezea hali ya kutisha: hali inaendelea kuzorota, aliandika, na katika miezi ya Novemba na Desemba kulishuhudiwa ongezeko kubwa la vurugu na mauaji.

Hali hii imezorota zaidi baada ya kuibuka kwa makundi ya waasi kama vile Forebu na RED-Tabara. Mapigano kati ya makundi haya na vikosi vinavyomuunga mkono rais Pierre Nkurunziza yamesababisha maafa makubwa. Sababu kubwa: Wafadhili wanazidi kuitenga Burundi, na hali hiyo inasababisha Burundi kuendelea kutumbukia katika mdororo mkubwa wa kiuchumi ambapo raia ndio wanaendelea kuathirika zaidi, pamoja na uhaba wa chakula na dawa.

Mkuu wa operesheni za kulinda amani hatimaye amezungumzia mazingira matatu ambao yanaweza kutokea kwa wakati wowote nchini Burundi: machafuko ambayo Umoja wa Mataifa unaweza kudhibiti kupitia mazungumzo ya kisiasa na kuunga mkono Umoja wa Afrika; kuongezeka kwa vurugu na hatari ya kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe; na hatimaye, tukio baya zaidi, ni mauaji ya kimbari. Katika matukio haya mawili ya mwisho, Umoja wa Mataifa unapaswa kupeleka kikosi cha askari wa kulinda amani. Lakini Hervé Ladsous anakiri kuwa bila msaada wa nchi wanachama, Umoja wa Mataifa kwa sasa utakuwa hauna nguvu ili kuhakikisha ulinzi wa raia wa Burundi.