BURUNDI-JARIBIO LA MAPINDUZI

Burundi: Mahakama yatoa uamuzi dhidi ya watuhumiwa wa jaribio la mapinduzi

Cyrille Ndayirukiye (wa 2 kutoka kushoto) mbele ya Mahakama ya Rufaa ya mjini Gitega kabla ya kusikilizwa uamu dhidi ya watuhumiwa wa jaribio la mapinduzi, Januari 15, 2016.
Cyrille Ndayirukiye (wa 2 kutoka kushoto) mbele ya Mahakama ya Rufaa ya mjini Gitega kabla ya kusikilizwa uamu dhidi ya watuhumiwa wa jaribio la mapinduzi, Januari 15, 2016. © Griff Tapper / AFP

Wanajeshi na askari polisi ishirini na nane wameripoti Ijumaa hii mbele ya Mahakama mjini Gitega katikati mwa Burundi. Wanajeshi na askari polisi hao wamepatikana na hatia ya kuhusika katika jaribio la mapinduzi la Mei 13 na 14, 2015.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huo kulikua kukifanyika maandamano dhidi ya muhula wa tatu wa Rais Nkurunziza, maandamnao ambayo yalivunjwa na vikosi vya usalama kwa kutumia nguvu kupita kiasi. Watuhumiwa saba wameachiwa huru, 21 wamehukumiwa na Mahakama Kuu, wanne wamehukumiwa kifungo cha maisha jela.

Mwendesha mashitaka alikuwa aliomba kifungo cha maisha jela kwa watuhumiwa wote ishirini na nane, lakini ombi hilo limetekelezwa kwa maafisa waandamizi wanne wa ngazi ya juu katika jeshi na polisi, ikiwa ni pamoja na Cyrille Ndayirukiye, aliyekuwa waziri wa ulinzi na namba mbili katika jaribio la mapinduzi yaliyoshindwa Mei 13 na 14. Namba moja, Godefroid Niyombare, bado yuko mafichoni na hajakamatwa, ikiwa ni pamoja na viongozi wengine kadhaa wa jaribio la mapinduzi.

Wanasheria wanne wa wanajeshi na askari polisi hao waliohusika katika jaribio la mapinduzi walipingwa na mahakama, na watuhumiwa waliamua kujitetea peke yao. Cyrille Ndayirukiye alisema kuwa alifanya hivo "kwa kutetea Mkataba wa amani na maridhiano wa Arusha" wakati ambapo "askari polisi walikuwa wakiua raia."

Akikubali na kutetea jaribio hilo la mapinduzi, jenerali Cyrille Ndayrukiye alisema: "Siningeweza kulea mikono wakati ambapo askari polisi walikua wakiuawa raia, huku Nkurunziza akicheza mpira."

Mashahidi waliosikiliza uamzi huo wa Mahakama wamethibitisha kwamba licha ya hukumu dhidi yao, watuhumiwa hao wanne, majemadari wawili kutoka jeshi la zamani lililokua likiundwa na idadi kubwa ya Watutsi na wengine wawili kutoka kundi la zamani la waasi wa Kihutu CNDD-FDD, ambo wanaongoza nchi kwa sasa, waliondoka Mahakamani wakitabasamu, huku wakipata faraja na uungwaji mkono kutoka kwa familia zao pamoja na watu wengine waliokuwa wamekuja kusikiliza uamzi wa Mahakama.

Mashtaka matatu yametangazwa dhidi yao: jaribio la mapinduzi, mauaji ya wanajeshi, askari polisi na raia pamoja na uharibifu wa majengo.

Maafisa wa polisi tisa wahukumiwa kifungo cha mika thelathini jela

Maafisa tisa wa polisi na jeshi wamehukumiwa miaka thelathini jela kwa kushirikiana katika jaribio la mapinduzi. Wamepigwa marufuku pia kushikilia wadhifa wowote serikalini kwa kipindi cha miaka kumi.

Watuhumiwa wanane wengine wamehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kuhusika na makosa madogo, na wengine saba wamechiwa huru.