Burundi: visa vya mauaji vyaendelea kushuhudiwa Bujumbura

Wakazi wakiangalia mwili wa mtu aliyeuawa katika wilaya ya Nyakabiga, Bujumbura, Desemba 12, 2015.
Wakazi wakiangalia mwili wa mtu aliyeuawa katika wilaya ya Nyakabiga, Bujumbura, Desemba 12, 2015. © REUTERS/Jean Pierre Aime Harerimana

Nchini Burundi, hali ya sintofahamu imeendelea kuripotiwa, hasa katika maeneo mbalimbali ya mji wa Bujumbura, kutokana na visa mbalimbali vinavyoshuhudiwa ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakazi na mateso mengine wanayowakumba raia.

Matangazo ya kibiashara

Watu watatu wameuawa na wengine wengi wamejeruhiwa Jumatatu hii jioni katika mtaa wa 6 namba 89 tarafani Bwiza, baada ya watu wasiojulikana waliokua kwenye pikipiki kuwashambulia watu hao kwa risasi.

Sehemu hiyo kulikotokea shambulio imekua ikilengwa na mashambulizi mbalimbali hivi karibuni, na tayari watu kadhaa wamepoteza maisha kutokana na mashambulizi hayo na wengine sasa wamepoteza baadhi ya viungo vya mwili.

Katika shambulio la Jumatatu jioni, watu watatu, ikiwa ni pamoja na afisa wa polisi wa cheo cha juu, afisa mwandamizi katika wizara ya Elimu na mwanasheria mmoja wameuawa.

Msemaji wa polisi, Pierre Nkurukiye, ameelezea masikitiko yake kuona visa vya mauaji vimekithiri katika maeneo mbalimbali, hususan katika baadhi ya maeneo ya mji wa Bujumbura.

Hata hivyo polisi imekua ikiendelea na operesheni yake ya kamata kamata katika maeneo mbalimbali ya nchi. Lakini maeneo yanayosakamwa sana na operesheni hiyo ni yale ambayo ni kitovu cha maandamano dhidi ya muhula watatu wa Rais Nkurunziza. Vijana ndio hasa wanalengwa na operesheni hiyo ya polisi. Mashahidi wanasema baadhi ya wanaokamatwa huukotwa maiti siku chache baadaye.

Mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu yamekua yakiinyooshea polisi kidolea cha lawama kuhusika na visa hivyo vya mauaji ya vijana wanao kamatwa na baadaye kuokotwa maiti.

Wakazi wa mji wa Bujumbura wanasema wanatiwa hofu na kukithiri kwa mauaji hayo ambayo wanaona kuwa yanaweza kusababisha kutokea kwa mauaji ya kimbari au kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hata hivyo mpaka sasa serikali bado imeendelea kukataa kushiriki mazungumzo na muungano unaojumuisha wapinzani waliokimbilia nje ya nchi (CNARED), muungano ambao serikali inasema unaundwa na watu waliohusika katika jaribio la mapinduzi lililoshindwa Mei 13 na 14 mwaka 2015.