BURUNDI UASI-USALAMA

Burundi: Jenerali Niyombare ateuliwa kuongoza kundi la waasi

Kundi jipya la waasi nchini Burundi FOREBU lililoundwa hivi karibuni kwa minajili ya kumtimua madarakani Rais Pierre Nkurunziza, limetangaza kumteua Alhamisi hii Januari 21 jenerali Godefroid Niyombare kuliongoza kundi hilo.

Jenerali Godefroid Niyombarealiyeongoza jaribio la mapinduzi ya kijeshi yaliotibuliwa, Mei 13 hadi jioni.
Jenerali Godefroid Niyombarealiyeongoza jaribio la mapinduzi ya kijeshi yaliotibuliwa, Mei 13 hadi jioni. REUTERS/Jean Pierre Aime Harerimana
Matangazo ya kibiashara

Jenerali Godefroid Niyombare aliongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyotibuliwa jioni ya tarehe 13 Mei mwaka 2015 nchini Burundi.

Jenerali Niyombare, mwenye umri wa miaka 47, alikuwa mshirika wa karibu wa Pierre Nkurunziza, kiongozi wa zamani wa kundi la waasi wa kihutu CNDD-FDD (1993-2006) wakati wa vita vya maguguni vilivyokua vikiendeshwa na kundi hilo dhidi ya majeshi ya Burundi.

Jenerali Niyombare alikua kiongozi wa kwanza wa majeshi ya Burundi kutoka kabila la Wahutu (2009-2013), kisha mkuu wa idara ya taifa ya Ujasusi (SNR) kati ya mwezi Desemba 2014 na mwezi Machi 2015 alipofutwa kazi. "Uratibu wa kundi la waasi la FOREBU unasimamiwa na jenerali Godefroid Niyombare", msemaji mpya wa kundi hilo jenerali Edouard Niragira ametangaza ambapo sauti yake iliyorekodiwa imetumwa kwenye ofisi ya shirika la habari la Ufaransa AFP.

Jenerali Edouard Nibigira, afisa mwandamizi wa cheo cha juu katika polisi aliwahi kuhudumu kama mkurugenzi wa polisi inayopambana na Majanga.

Jenerali Niyombare tangu mwezi Novemba anakabiliwa na vikwazo vya Marekani, pamoja na kiongozi namba mbili wa mapinduzi Cyrille Ndayirukiye aliyekamatwa na kuhukumiwa hivi karibuni kifungo cha maisha jela.

Kanali Jules Ndihokubwayo, kutoka kundi la zamani la waasi la CNDD-FDD, ambaye aliwahi kuhudumu katika kitengo cha mawasiliano katika kikosi cha wanajeshi wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) na ambaye hivi karibuni alilitoroka jeshi la Burundi, ameteuliwa kuwa mkuu wa majeshi ya kundi la waasi la FOREBU. Anashirikiana na Luteni Kanali Edouard Nshimirimana, mpaka sasa msemaji wa kundi hili jipya la waasi, ambaye amethibitisha kwa AFP taasisi hizo mpya za kundi hilo.

Burundi imetumbukia katika mgogoro mkubwa wenye machafuko tangu mwezi Aprili, kufuatia uamuzi wa Pierre Nkurunziza wa kutangaza kuwania muhula wa tatu kwenye kiti cha urais. Uamuzi ambao kwa mujibu wa wapinzani wake, unaukiuka Katiba na Mkataba wa Amani na Maridhiano wa Arusha uliomaliza vita vilivyodumu zaidi ya mwongo mmoja kati ya makundi ya waasi na jeshi, ambalo wakati huo lilikua likiundwa na idadi kubwa ya Watutsi na makundi ya waasi yaliokua yakiundwa na Wahutu.

Kundi hili jipya la waasi linatafuta kuunganisha makundi yote ya waasi ili waweze kumn'goa madarakani Rais Pierre Nkurunziza, afisa wa FOREBU, ambaye hakutaka jina lake litajwe ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP. "Sio mshangao kuona tangazo hili linatolewa sanjari na kuwasili kwa (ujumbe) wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini Bujumbura", ameongeza afisa huyo.

Upande wa serikali hawajazungumzia chochote kuhusu tangazo hili.

Hayo yakijiri hali ya wasiwasi inaendelea kutanda katika maeneo mbalimbali nchini Burundi, hasa mjini Bujumbura, ambapo polisi imeendelea na operesheni yake ya kamata kamata, huku vijana wakilengwa zaidi.