TANZANIA-RUSHWA

Rais wa Tanzania awasimamisha kazi maafisa wakuu wa uhamiaji

John Pombe Magufuli, Rais mpya wa Tanzania, Oktoba 30, 2015.
John Pombe Magufuli, Rais mpya wa Tanzania, Oktoba 30, 2015. REUTERS/Sadi Said

Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amewasimamisha kazi maafisa wawili wa uhamiaji mara moja hadi uchunguzi utakapokamilika.

Matangazo ya kibiashara

Maafisa waliosimamishwa kazi ni pamoja na Kamishna Mkuu wa Uhamiaji nchini humo Sylvester Ambokile na Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia Utawala na fedha Bw Piniel Mgonja. Wote hao wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi katika idara ya uhamiaji.

Taarifa kutoka Idara ya mawasiliano ya ikulu imesema Ambokile amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali zinazohusiana na rushwa, ukusanyaji mbaya wa maduhuli ya serikali, ukiukwaji wa taratibu za manunuzi na utendaji mbovu.

Tuhuma hizo zilibainika wakati waziri wa mambo ya ndani ya nchi Bw Charles Kitwanga alipotembelea idara ya uhamiaji hivi karibuni

“Kama watabainika kutokuwa na hatia ya makosa wanaotuhumiwa, basi Rais ataamua hatima yao,” Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema watendaji hao wakuu wa uhamiaji wamesimamishwa kazi mara moja hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.

“Rais Magufuli amefanya mabadiliko hayo kwa lengo la kumtafuta mtu mwenye utaalamu wa kuendeleza kazi iliyofanywa na Bw Maswi”, Bw Sefue ameongeza.

Tangu kuchukua madaraka mwezi Novemba mwaka jana, Dkt Magufuli amewasimamisha au kuwafuta kazi maafisa wakuu kadhaa serikalini.

Itafahamika kwamba hivi karibuni Rais John Pombe Magufuli aliwafuta kazi maafisa wengine mbalimbali ikiwa ni pamoja na mkuu wa kupambana na rushwa, afisa mkuu wa reli na alivunja bodi ya bandari Tanzania.