BURUNDI-WANAHABARI WA KIGENI

Burundi: waandishi wawili wa habari wa "Le Monde" wakamatwa

Polisi katika mitaa ya Musaga, jijini Bujumbura, mji mkuu wa Burundi, Julai 24 2015.
Polisi katika mitaa ya Musaga, jijini Bujumbura, mji mkuu wa Burundi, Julai 24 2015. REUTERS/Mike Hutchings

Nchini Burundi, polisi imetangaza kukamatwa kwa waandishi wa habari wawili wa kigeni. Wanahabari hao Jean-Philippe Rémy, na mpiga picha wa Uingereza Phil Moore, ambao wote wanafanya kazi katika shirika la habari la Ufaransa AFP na gazeti la Le Monde.

Matangazo ya kibiashara

Habari hii imethibitishwa na Willy Nyamitwe, mshauri mkuu wa wa Rais Pierre Nkurunziza anayehusika na mawasiliano. Watu wengine kumi na tano wamekamatwa wakati wa operesheni ya polisi.

Kwa ujumla, watu kumi na saba wamekamatwa katika wilaya za Nyakabiga na Jabe, ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari wawili wa kigeni.

"Jambo la ajabu, kwa mara ya kwanza, raia wa kigeni, ambao wana kibali kinachowaruhusu kufanya kazi nchini Burundi kama waandishi wa habari wamejikuta miongoni mwa wahalifu waliokamatwa", Moise Nkurunziza, mmoja wa wasemaji wa polisi amesema kwenye runinga ya taifa. Moise Nkurunziza amesema kuwa silaha kadhaa zimekamatwa wakati wa operesheni ya polisi: silaha ya kurusha bomu, Kalashnikov na bastola. Msemaji huyo wa polisi ameeleza kuwa operesheni hiyo imeendeshwa kwa msaada wa mtu mmoja kati ya raia anayeshirikiana na polisi.

Taarifa hii imethibitishwa kwenye Twitter na Willy Nyamitwe, mshauri mkuu wa Rais Pierre Nkurunziza anayehusika na mawasiliano.

Wakati wa mchana mkazi mmoja wa wilaya ya Jabe aliifahamisha RFI kuna operesheni ya polisi ambayo inafanyika katika wilaya za Jabe na Nyakabiga.

Jean-Philippe Rémy ni mwandishi wa habari mahiri na anayetambua vizuri Afrika. Anaongoza ofisi ya kikanda ya gazeti la Le Monde katika mji wa Johannesbroug nchini Afrika Kusini. Aliwasili nchini Burundi tarehe 19 Januari mwaka 2016. Tayari aliingia nchini Burundi mara kadhaa kufanya kazi yake ya uandishi wa habari, ikiwa ni pamoja na tangu mwanzoni mwa machafuko.

Kwa upande wake Phil Moore ni mpiga picha wa kujitegemea, kulingana na tovuti yake. Phil Moore ana umri wa miaka 36, anaishi katika mji wa Berlin, nchini Ujerumani. Anafanya kazi kwa vyombo vya habari kadhaa vya Ufaransa na vya kimataifa.