AFRIKA KUSINI

Afrika Kusini: wabunge wakutana kujadili hatima ya Zuma

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma mbele ya Bunge.
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma mbele ya Bunge. REUTERS/Schalk van Zuydam/Pool

Wabunge nchini Afrika kusini wanakutana hii leo kujadili hoja ya kutokuwa na imani na rais wa nchi hiyo Jacob Zuma, kabla ya kuipigia kura wakati huu upinzani nchini humo ukiendelea kumshinikiza bwana Zuma kujiuzulu, kufuatia tuhuma za ufisadi zinazomkabili.

Matangazo ya kibiashara

Zuma anatuhumiwa kufanya ubadhirifu wa Euro milioni 15 fedha za umma kwa ajili ya kuifanyia ukarabati nyumba yake binafsi iliyopo katika eneo la Nkandla mashariki mwa nchi hiyo.

Vyama vya upinzani nchini Afrika Kusini ndivyo vilivyomfungulia kesi Zuma kutokana na hatua yake ya kutumia vibaya fedha za umma.

Hivi karibuni Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini ilithibitisha kutumiwa kiasi cha Euro milioni 15 kwa ajili ya kukarabari nyumba binasfi ya Rais Jacob Zuma kukiwemo kuimarisha hali ya usalama wa nyumba hiyo, kujenga bwawa la kuogolea, ukumbi wa michezo ya kuigiza na kadhalika.

Zuma amekataa kurejesha fedha hizo na kujifanya kutokuwa na taarifa kuhusu kitita hicho cha fedha.