DRC-MAUAJI-USALAMA

DRC: watu 13 wauawa katika shambulio la ADF Beni

Wanajeshi wa Monusco, Oktoba 13, 2014 Béni DRC.
Wanajeshi wa Monusco, Oktoba 13, 2014 Béni DRC. AFP PHOTO / ALAIN WANDIMOYI

Maafisa wakuu wa jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamethibitisha kuuawa kwa watu 13 katika mashambulizi ya silaha, yanayodaiwa kutekelezwa na waasi wa Uganda wa kundi la ADF katika kijiji cha Mambabio-Ntombi wilayani Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Matangazo ya kibiashara

Kamanda wa jeshi anayeongoza operesheni inayofahamika kama Sokola I, Jenerali Marcel Mbangu, amesema mbali na silaha waasi hao walitumia visu na marungu, wakati wa mashambulizi yao, usiku wa kuamkia jumatatu hii.

Jenerali Mbangu anasema waasi hao wa ADF pia walikivamia kituo kimoja cha afya ambapo walipora dawa kabla ya kumjeruhi muuguzi.
Kwa upande wake Msemaji wa jeshi la Congo FARDC, Mak Hazukai, amethibitisha kupelekwa kwa kikosi cha msaada wa dharura kukabiliana na kundi hilo.

Wakati hayo ya kijiri serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetupilia mbali wito kutoka kwa baadhi ya nchi za Magharibi ambazo zinasema hukumu ya kifungo cha miaka miwili jela iliyotolewa na mahakama dhidi ya wanaharakati sita mjini Goma iangaliwe upya.

Kauli hiyo inafuatia ombi la Ufaransa na Ubelgiji ambao siku ya Alhamisi iliyopita, pia wameiomba Congo kuheshimu uhuru wa kujieleza na kuhakikisha amani ya kidemokrasia inazingatiwa.

Wakati huo huo, kampeni ya uchaguzi wa magavana imeanza nchini humo ambapo serikali imekosoa ujanja wa baadhi ya wagombea huru kukiuka maadili ya uchaguzi.