SOMALIA-MAREKANI-AL SHABAB-UGAIDI

Somalia: Marekani yaangamiza "wapiganaji zaidi ya 150" wa Al Shebab

Ndege isio na rubani ya Marekani ikitua kwenye uwanja wa ndege wa Jalalabad, Afghanistan, ambapo ndege ya kijeshi ya Marekani aina ya C-130 ilianguka, Oktoba 2,2015.
Ndege isio na rubani ya Marekani ikitua kwenye uwanja wa ndege wa Jalalabad, Afghanistan, ambapo ndege ya kijeshi ya Marekani aina ya C-130 ilianguka, Oktoba 2,2015. AFP PHOTO / Noorullah Shirzada

Marekani ikitumia ndege isio na rubani imewaua "zaidi ya wapiganaji 150" wa Al Shabab Jumamosi Machi 5 ambao walikua wameandaa mashambulizi ya "kiwango cha juu" kutoka kambi ilio kwenye umbali wa kilometa 200 kaskazini mwa mji wa Mogadishu, Pentagon imesema Jumatatu hii.

Matangazo ya kibiashara

"Wapiganaji wa (Al Shabab) walikuwa wakifanya mafunzo kwa ajili ya mashambulizi ya kiwango cha juu. Walikuwa katika hatua ya kuondoka kambini na walikiua tishio kubwa kwa Marekani na vikosi vya Umoja wa Afrika", msemaji wa Pentagon, Jeff Davis, amesema.

"Kulingana na ripoti ya kwanza, zaidi ya wapiganaji 150 wapiganaji wa kigaidi wameangamizwa," Bw Davis ameeleza.

Wapiganaji wa Al Shabab, kundi lenye uhusiano na Al Qaeda, wameongeza mashambulizi kwa kiwango cha juu tangu mwanzoni mwa mwaka huu nchini Somalia.

Wapiganaji wanaolengwa na Washington walikuwa katika hatua ya kumaliza mafunzo yatakayowaruhusu kuendesha "operesheni kabambe," Davis ameongeza, bila kufafanua aina ya mashambulizi yaliyopangwa na wapiganaji wa Al Shabab.

"Kuangamizwa kwao kutapunguza uwezo wa kundi la Al Shabab kwa kufikia malengo yao nchini Somalia, kama vile kuajiri wapiganaji wapya, kuanzisha kambi mpya, na kupanga mashambulizi dhidi ya vikosi vya Marekani na vile vya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM)," mwakilishi wa wizara ya Ulinzi ya Marekani amebainisha.

Kambi hii ya mafunzo ilikuwa ikifuatiliwa kwa muda fulani. "Kulikuwa na hisia kwamba hatua ya utendaji ilikua mbioni kutekelezwa," kwa mujibu wa Bw Davis.

Baada ya kutimuliwa mjini Mogadishu mwezi Agosti mwaka 2011, wapiganaji wa Al Shabab wamekabiliwa na upungufu fulani. Walikuwa wamepoteza ngome zao kuu, hata kama wamekua wakishika udhibiti wa maeneo mengi ya vijijini.