TUNISIA-MAANDAMANO-MAPIGANO

Tunisia: mapigano yatokea katika mpaka wa Libya

Vikosi maalum vya Tunisia wakati wa shambulio, katika mji wa Ben Guerdane karibu na mpaka wa Libya, Machi 7, 2016.
Vikosi maalum vya Tunisia wakati wa shambulio, katika mji wa Ben Guerdane karibu na mpaka wa Libya, Machi 7, 2016. © FATHI NASRI / AFP

Nchini Tunisia, kumetokea mapigano mapya kati ya vikosi vya usalama na watu wanaoshukiwa kuwa magaidi. Shambulizi hilo limetokea mapema Jumatatu hii alfajiri katika mji wa Ben Guerdane kusini mwa nchi, kwenye mpaka na Libya.

Matangazo ya kibiashara

Katika mapigano hayo, washambuliaji 28 wameuawa, ikiwa ni pamoja na askari polisi 10 na raia saba. Rais wa Tunisia amelaani shambulizi hilo ambalo amelitaja kuwa la kigaidi.

Mji wa Ben Guerdane unakumbwa na mfululizo wake wa pili wa vurugu ndani ya siku sita. Katika mji huo, wakazi wanasema kuwa hali ni tete laikini imedhibitiwa na vikosi vya usalama, huku wanajeshi zaidi wakipekwa kwenye eneo la shambulizi.

Hili ni tukio jipya ambalo limetokea nchini Tunisia : mapema alfajiri, watu wenye silaha wameshambulia kwa wakati mmoja kambi ya askari polisi, lakini pia vituo vya polisi na vikosi vya ulinzi wa taifa katika mji huu wa Ben Guerdane, kilomita thelathini kutoka kwenye mpaka wa Libya. Majaribio hayo yametibuliwa na kufuatiwa na urushianaji risasi kati ya washambuliaji na vikosi vya usalama mbele ya umati wa watu ambao walikuja kusaidia vikosi vya jeshi. Serikali imemetoa wito kwa wakazi kuondoka eneo hilo la mashambulizi ili kuzuia vifo vya raia. Kufuatia shambulio hilo, amri ya kutotoka nje imetangazwa na serikali katika mji wa Ben Guerdane.

Uchunguzi umeanzishwa. Vikosi vya usalama sasavitawahoji watuhumiwa sita ambao walikamatwa. Wachunguzi pia watajaribu kujua kama watu hawa waliingia nchini Tunisia wakitokea Libya.

Jumatano iliyopita, watu watano wanaoshukiwa kuwa magaidi waliuawa katika jimbo la Ben Guerdane. Serikali ya Tunisia iko katika hali ya tahadhari.