COTE D'IVOIRE-ETOILE DU SUD-MAUAJI

Côte d'Ivoire: zaidi ya watu 12 wauawa Grand Bassam

Rais wa Côte d'Ivoire, Alassane Ouattara, katika mji wa Grand Bassam siku ya Jumapili Machi 13.
Rais wa Côte d'Ivoire, Alassane Ouattara, katika mji wa Grand Bassam siku ya Jumapili Machi 13. © REUTERS/Luc Gnago

Shambulizi la Jumapili hii katika mji wa kitalii wa Grand-Bassam nchini Côte d'Ivoire limegharimu maisha ya raia kumi na wanne na askari wawili wa vikosi maalumu, Rais wa Côte d'Ivoire Alassane Ouattara amesema.

Matangazo ya kibiashara

Washambuliaji sita pia wamepoteza maisha katika mji huo wa mapumziko, kilomita arobaini mashariki mwa mji wa Abidjan.

Shambulio hili limetokea katika hoteli inayofahamika kwa jina la Etoile du Sud, inayopatikana katika pwani ya mji wa Bassam.

Kwa mujibu wa chanzo cha kijeshi, watu watano wanasadikiwa kuwa wameuawa na zaidi ya wengine kumi na mbili kujeruhiwa. Watu waliojeruhiwa wamesafirishwa katika mji wa Abidjan. Lakini kwa mujibu wa mashahidi, idadi ya watu waliouawa inaweza kuwa kubwa, kati ya saba na tisa.

Katika hotuba yake kwa taifa, Rais wa Côte d'Ivoire, Alassane Ouattara amesema raia 14 na askari 2 wameuawa katika shambulio la Grand Bassam.

Washambuliaji walioelezwa na shahidi aliyenukuliwa na shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa wana "silaha za kivita" bado hawajajulikana kwa wakati huu.

Awali, shahidi mmoja alizungumza kwamba risasi zilikua zikirushwa zikitokea katika eneo la pwani, karibu na eneo la hoteli. Lakini baadae alisema kuwa walipata taarifa kuwa risasi zilikua zikipigwa katika hoteli ya Etoile du Sud, iliyoko katika mtaa uliobatizwa kwa jina la vyombo vya Sheria, amearifu mwandishi wa RFI katika mji wa Grand Bassam.

Magari ya kijeshi, yakibeba bunduki za kivita, na wawindaji wa jadi wanaojulikana kwa jina la Dozo waliokua wakibebelea silaha, pia walikua wakielekea katika eneo la shambulizi.

Mji wa kihistoria na mji mkuu wa zamani wa Côte d'Ivoire katika pwani ya Ghuba ya Guinea, Grand-Bassam ina hoteli kadhaa zinazotembelewa na watu kutoka nchi za kigeni hasa nchi za magharibi.

Kundi la AQMI, lenye mafungamano na Al Qaeda limekiri katika tovuti yake kuhusika na shambulizi hilo.

Askari wa Côte d'Ivoire mbele ya hoteli ya Etoile du Sud wakiwalenga wauaji wenye silaha Jumapili hii Machi 13, 2016.
Askari wa Côte d'Ivoire mbele ya hoteli ya Etoile du Sud wakiwalenga wauaji wenye silaha Jumapili hii Machi 13, 2016. REUTERS/Luc Gnago