BURUNDI-RWANDA-DIPLOMASIA

Mamlaka ya Burundi yadai kumkamata askari wa Rwanda

Maiti zikiokotwa katika mitaa ya Bujumbura asubuhi ya Desemba 12, 2015.
Maiti zikiokotwa katika mitaa ya Bujumbura asubuhi ya Desemba 12, 2015. © REUTERS/Jean Pierre Aime HarerimanaTEMPLATE OUT

Nchini Burundi, polisi inadai kuwa imemkamata "jasusi" wa Rwanda. Vyombo vya usalama nchini humo vilimuonyesha mbele ya vyombo vya habari Jumamosi hii mchana vikidai kuwa ni askari wa Rwanda aliyetumwa Burundi kufanya upelelezi.

Matangazo ya kibiashara

Inadaiwa kuwa mtu huyo alikamatwa Jumatatu Machi 7 katika kijiji cha Rushenya, Kaskazini mashariki mwa Burundi kwenye mpaka na Rwanda. Vikosi vya usalama vya Burundi vinabaini kwamba mtu aliekamatwa ni askari wa Rwanda alietumwa kuzorotesha usalama wa nchi hiyo.

Mtu anayedaiwa kuwa askari wa Rwanda alionyeshwa mbele ya vyombo vya habari akiwa katika majengo ya Idara ya Ujasusi ya Burundi (SNR), ambapo alikua hafungwi pingu na wala hakua na dalili dhahiri za majeraha na inaonekana kuwa hajafanyiwa kipigo, kama wanavyokamayiwa watu wengine ambao wanatuhumiwa makosa yanayohusiana na mdororo wa usalama nchini humo.

Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa polisi ameelezea uraia wa mtuhumiwa huyo, namba yake ya jeshi na kuhakikisha kwamba ni askari wa Rwanda alietumwa kufanya upelelezi nchini Burundi.

Madhumuni ya kuja kwake nchini Burundi, kwa mujibu wa vikosi vya usalama, ilikuwa kuomba msaada kwa watawa katika mkoa wa Muyinga kwa kuweza kuwaficha wapiganaji 200, ambao wangeliendesha mashambulizi nchini Burundi. Mtu huyo hatimaye alikamatwa na polisi.

Mtu huyo mwenye umri wa miaka 30, anayeadiwa kuwa askari wa Rwanda si mara ya kwanza kuingia katika ardhi ya Burundi. Pia kwa mujibu wa polisi, mtu huyo anasadikiwa kuwa aliingia mara mbili nchini Burundi mwaka 2015. Kwa mara ya kwanza alijaribu kuwasafirisha askari waliohusika katika jaribio la mapinduzi lililoshindwa mwezi Mei 2015. Mara ya pili aliingia nchini Burundi kukusanya taarifa katika lengo la kutekeleza " mashambulizi dhidi ya viongozi wakuu nchini Burundi ".

Jumamosi hii, wakati alionyeshwa katika ukumbi wa SNR, Idara ya Ujasusi inayotuhumiwa kuwatendea watu mateso mbalimbali na mauaji kwa watu ambao wako mikononi mwa vyombo vya dola, mtu huyo anaedaiwa kuwa askari wa Rwanda, alikiri kuingia Burundi kwa lengo la kufanya upelelezi.

Huu ulikua ujumbe wake wa tatu nchini Burundi ambao ulikua unalenga kuvuruga usalama wa nchi, amesema msemaji wa polisi Pierre Nkurikiye.

Tangu kuanza kwa mgogoro wa kisiasa nchini humo, mahusiano yameendelea kudorora kati ya Burundi na Rwanda. Serikali ya Burundi inaishtumu Rwanda kuwapa mafunzo ya kijeshi katika ardhi yake wakimbizi wa Burundi kwa lengo la kuhatarisha usalama wa taifa. Tuhuma ambazo seikali ya Rwanda inafutilia mbali.

Serikali ya Rwanda hadi sasa haijajibu kuhusu taarifa hii ya kukamatwa kwa askari wake lakini mapema Jumamosi, Rais wa Rwanda Paul Kagame alikanusha kwa mara nyingine kwamba nchi yake haingilii kamwe masuala ya ndani ya Burundi.