NIGER-HAMA-SHERIA

Niger: Hama Amadou aondolewa jela

Bango la kampeni la Bw Hama Amadou, Niamey, Februari 2, 2016.
Bango la kampeni la Bw Hama Amadou, Niamey, Februari 2, 2016. © BOUREIMA HAMA / AFP

Hatimaye ni habari njema kwa ndugu na wafuasi wa kiongozi mkuu wa upinzani nchini Niger Hama Amadou. Kiongozi huyu wa upinzani nchini Niger ameondolewa katika jela la Filingué ambapo alikuwa akizuiliwa kwa tuhuma ya biashara ya mtoto.

Matangazo ya kibiashara

Hama Amadou amesafirishwa katika helikopta, kabla ya kutua katika mji mkuu wa Niger, Niamey, na Jumatano jioni amesafirishwa kwa ndege maalumu hadi nchini Ufaransa. Itakumbukwa kwamba, Hama Amadou alifuzu kwa duru ya pili ya uchaguzi wa rais, uliopangwa kufanyika Jumapili hii, Machi 20.

Daima mgombea wa chama cha Copa 2016 kwa uchaguzi wa Jumapili hii, Hama Amadou amewasili katika mji mkuu wa Niger Jumatano hii, Machi 16. Tangu Jumatatu, alikuwa amelazwa hospitalini katika mji wa Filingué, baada ya afya yake kuzorota ghafla.

Awali daktari wake binafsi, kisha serikali ya Niger, walibaini kwamba Hama Amadou anakabiliwa na uchovu, na kuna haja ya kutibiwa katika kituo maalumu. Taarifa hii ilithibitishwa Jumanne na Waziri wa Sheria.

Waziri huyo amethibitisha Jumatano hii kwamba mgombea huyo, ambaye alikua akizuiliwa tangu mwezi Novemba mwaka jana anapaswa kusafirishwa kwa ndege maalumu. Kulingana na taarifa zetu, daktari wa Hama Amadou, ambaye ni raia wa Ufaransa, alitahadhari viongozi wa Ufaransa kuhusu kuzorota kwa afya ya mgombea huyo.

Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa, ndege ya Hama Amadou imeondoka Jumatano hii jioni mjini Niamey kwenda mjini Paris, nchini Ufaransa. Kwa mujibu wa daktari wake, Hama Amadou, aliyekua Spika wa Bunge la Niger anakabiliwa na ugonjwa sugu, ambapo anatakiwa kufuatiliwa kila baada ya miezi mitatu nchini Ufaransa katika Hospitali ya Marekani ya Neuilly-sur-Seine.

Kuhusu hali ya daktari binafsi wa Hama Amadou, aliyekamatwa Jumanne hii kwa kosa la "kutoa habari za uongo", bado anazuliwa katika majengo ya polisi. Profesa Yacouba alionya kuhusu kuzorota kwa hali ya mgonjwa.