Zanzibar - Uchaguzi

Mohamed Shein atangazwa mshindi Zanzibar

Rais mteule wa Zanzibar, Dr Ali Mohamed Shein, akionesha cheti alichokabidhiwa na tume ya uchaguzi Zanzibar, ZEC
Rais mteule wa Zanzibar, Dr Ali Mohamed Shein, akionesha cheti alichokabidhiwa na tume ya uchaguzi Zanzibar, ZEC RFIKISWAHILI

Tume ya Uchaguzi Visiwani Zanzibar ZEC, imemtangaza Ali Mohamed Shein kuwa mshindi wa marudio ya uchaguzi wa urais visiwani Zanzibar nchini Tanzania.

Matangazo ya kibiashara

Mwenyekiti wa tume hiyo Jecha Salim Jecha alitangaza kuwa rais Shein alishinda uchaguzi huo kwa asilimia 91 nukta 4 sawa na kura 299,982.

Kati ya wapiga kura 503,580 waliosajiliwa katika daftari la wapiga kura Visiwani humo, ni asilimia 67 nukta 9 sawa na 341,865 ndio waliojitokeza kushiriki katika uchaguzi huo uliosusiwa na chama kikuu cha upinzani CUF.

Kura 13,538 ziliharibika kwa mujibu wa Tume hiyo, huku kura halali zikiwa ni 328,327.

Mshindi wa pili Hamad Rashid kutoka chama chama cha ADC
alipata kura elfu 9 na ametoa wito kwa rais mteule Shein kushirikiana na kila mmoja ili kuunda serikali ya pamoja.

Baada ya kupokea cheti cha ushindi, rais Shein amesema atahakikisha kuwa kwa miaka mitano ijayo, anatenda haki kwa Wazanzibari wote.

“Nafahamu matatizo tuliyonayo, nafahamu kama jina langu kuwa kuna mgawanyiko wa kisiasa na nitafanya kazi na kila mmoja kuhakikisha kuwa tunafanikiwa,” alisema.

Aidha, ameahidi kuendelea kuimarisha uchumi wa Zanzibar lakini pia kuendelea kudumisha hali ya usalama visiwani humo.

“Nimejitolea kuwa rais wa Zanzibar ili kuhakikisha kuwa tunafanikiwa,”

“Nitasimamia umoja wa watu wa Zanzibar na sina cha kuwalipa kwa ushindi huu ,” aliongeza.

“Nina uhakika uchumi wa Zanzibar kwa miaka mitano ijayo utakuwa kati ya asilimia 8 na 10 kwa sababu tunataka kusitisha utegemezi,” alisisitiza.

Kipindi chote cha uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita, hali ya usalama iliimarishwa katika Kisiwa hicho huku maafisa wa usalama wakionekana wakipiga doria kila kona.

Waangalizi wa Umoja wa Afrika na wale kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki ndio walioshuhudia uchaguzi huo uliosusiwa na waangalizi kutoka Umoja wa Ulaya ya Mataifa mengine ya Magharibi waliosema hakukuwa na haja ya marudio ya uchaguzi huo kwa sababu ule wa mwaka jana ulikuwa huru na haki.

Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF Maalim Seif ambaye aliwania urais wa mwaka 2015 na kujitangazia ushindi, amesisitiza kutoyatambua marudio ya uchaguzi huo.