BURUNDI-MAUAJI-JESHI

Burundi: Afisa wa ngazi ya juu jeshini auawa kwa kupigwa risasi Bujumbura

Askari wa Burundi wakiondoka wilaya ya Cibitoke mjini Bujumbura, 1 Julai mwaka 2015.
Askari wa Burundi wakiondoka wilaya ya Cibitoke mjini Bujumbura, 1 Julai mwaka 2015. MARCO LONGARI / AFP

Mkuu wa kambi ya kijeshi ya Muzinda, Luteni Kanali Darius Ikurakure, ameuawa katika makao makuu ya jeshi mjini Bujumbura. Taarifa hii imethibitishwa na jeshi la Burundi. Afisaa huyo ameuawa wakati ambapo askari wengi wamekua wamejielekeza makwao.

Matangazo ya kibiashara

Afisaa huyo amekua akituhumiwa na upinzani pamoja na mashirika ya kiraia kujihusisha na uhalifu mbalimbali dhidi ya binadamu, hususan mauaji ya wafuasi wa upinzani, mateso kwa waandamanaji na mengineyo.

Luteni kanali Darius Ikurakure, alikua mmoja wa mafisa wa jeshi ambaye alikua mwaminifu kwa utawala wa Pierre Nkurunziza, baada ya kupewa majukumu ya kusimamia ulinzi na kuongoza majeshi katika maeneo ya kaskazini mwa mji wa Bujumbura (Cibitoke, Mutakura, Buterere na Ngagara) ambayo ni kitovu cha maandamano dhidi ya muhula wa tatu wa Rais Pierre Nkurunziza.

Mshauri mkuu wa rais anayehusika na mawasiliano, Willy Nyamitwe, ameyafananisha mauaji ya afisaa huyo kwenye Twitter kama yale yaliyotokea Jumanne hii mjini Brussels, nchini Ubelgiji, akibaini kwamba mauaji yote hayo yanaendana na ugaidi.

Mauaji ya afisaa huyo wa jeshi ni pigo kubwa kwa serikali pia kwa chama tawala CNDD-FDD, ambacho alipitia kwa kuwa mwanajeshi wa taifa, katika vita vya maguguni viliyodumu zaidi ya mwongo mmoja nchini Burundi.

Upinzani umekua ukimyooshea kidole cha lawama kwa mauaji mbalimbali ya wafuasi wake pamoja na mateso kwa waandamanaji waliopinga muhula watatu wa Rais pierre Nkurunziza.

Machafuko nchini Burundi yamesababidsha watu zaidi ya 400 kuawa kwa mujibu wa mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu, na wengine zaidi ya 200,000 kuyahama makaazi yao na kukimbila katika nchi jirani, hususan Tanzania, Rwanda, Jamhuri ya kidemokrasisa ya Congo, Uganda, Kenya, na Zambia.

Uchunguzi kuhusu mauaji ya Darius Ikurakure unaendelea, lakini mpaka sasa mtu aliyehusika na mauaji hayo hajabainika.