NIGER-SIASA-SERIKALI YA UMOJA

Niger: Rais Issoufou aomba upinzani kushirikiana

Rais wa Niger Mahamdou Issoufou autaka upinzani kushirikiana kwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Rais wa Niger Mahamdou Issoufou autaka upinzani kushirikiana kwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. REUTERS/Afolabi Sotunde/Files TPX IMAGES OF THE DAY

Rais Mahamdou Issoufou, aliyeshinda uchaguzi wa urais wa Jumapili Machi 20 nchini Niger, amesema yuko tayari kushirikiana na upinzani kwa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ili kukabiliana na masuala changamoto mbalimbali zinazowakabili raia wa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

"Niko tayari kuunda pamoja na upinzani serikali ya umoja wa kitaifa ili kukabiliana na vitisho ambavyo vinawakabili raia wa Niger. Hakuna changamoto tu ya usalama, kuna changamoto nyingine, kama vile changamoto ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Changamoto zote hizi zinahitaji muungano wa kitaifa," Rais wa Niger amesema katika mahojiano na shirika la habari la Ufaransa la AFP.

Rais Issoufou ametoa pendekezo hilo , siku moja tu baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais kwa zaidi ya 90% ya kura. Rais Issoufou amepata ushindi huo katika duru ya pili ya uchaguzi uliosusiwa na upinzani. Wagombea wawili ndio walikua walifaulu kuingia katika duru ya pili ya uchaguzi nchini Niger, ambao ni pamoja na mshindi wa uchaguzi huo Rais Mahamdou Issoufou na Hama Amadou, ambaye alisafirishwa juma lililopita nchini Ufaransa kwa ajili ya matibabu, baada ya afya yake kuzorota.

Hama Amadou alisafirishwa nchini Ufaransa saa chache baada ya kuachiliwa huru kutoka jela alipokua akizuiliwa baada ya duru ya kwanza ya uchaguzi.

Awali daktari wake binafsi, kisha serikali ya Niger, walibaini kwamba Hama Amadou anakabiliwa na uchovu, na kuna haja ya kutibiwa katika kituo maalumu. Taarifa hii ilithibitishwa Jumanne juma lililopita na Waziri wa Sheria.

Siku moja baadaye Waziri wa Sheria alithibitisha kwamba mgombea huyo, ambaye alikua akizuiliwa tangu mwezi Novemba mwaka jana anapaswa kusafirishwa kwa ndege maalumu. Kulingana na taarifa zetu, daktari wa Hama Amadou, ambaye ni raia wa Ufaransa, alitahadhari viongozi wa Ufaransa kuhusu kuzorota kwa afya ya mgombea huyo.