COTE D'IVOIRE-MAKABILIANO-MAUAJI

Côte d'Ivoire: zaidi ya watu 20 wauawa katika makabiliano Bouna

Mfugaji wa ng'ombe, Côte d'Ivoire.
Mfugaji wa ng'ombe, Côte d'Ivoire. © Getty Images/Eco Images

Watu wasiopungua 20 waliuawa baada ya makabiliano ya siku mbili katika eneo la Bouna, kaskazini mashariki mwa Côte d’Ivoire Alhamisi Machi 24 na Ijumaa Machi 25.

Matangazo ya kibiashara

Mgogoro kati ya wakulima na wafugaji ulizua hali ya sintofahamu katika eneo hilo. Ili kudhibiti hali ya mambo na kurejesha utulivu, majeshi yametumwa kwa wingi katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, ni kitendo cha kulipiza kisasi kiliozua hali ya taharuki: uchomaji wa gari. Alhamisi asubuhi katika mji wa Bouna, mgogoro unaodumu miaka kadhaa kati ya wakulima kutoka jamii ya Lobi na wafugaji kutoka jamii ya Peul ulizuka na kusababisha hali ya wasiwasi katika eneo la Bouna.

Wakulima wanawashtumu wafugaji kuharibu mimea yao kwa kulisha mifugo yao. Wakijihami kwa mapanga na bunduki, jamii hizi mbili zilikabilian vikali katika mji wa kaskazini mashariki mwa Côte d’Ivoire na viunga vyake. Kwa uchache watu 20 waliuawa na thelathini walijeruhiwa kwa mujibu wa vyanzo kutoka eneo hilo. Soko limechomwa.

Baadhi ya wakimbizi 2 000 wakimbilia katika kambi ya ONUCI

Kutokana na hofu, wakazi wa eneo hilo walikimbia: baadhi nyumbani kwa mkuu wa mji wa Bouna, wengine katika kambi ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Côte d’Ivoire (ONUCI). Kwa mujibu wa msemaji wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Côte d’Ivoire, watu 2 000 wamekimbilia katika kambi hiyo. Chakula na madawa vimemetumwa huko.

Majeshi ya kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Côte d’Ivoire wametumwa kwa wingi katika kambi hiyo: zaidi ya askari mia moja wa kulinda amani kutoka Senegal na askari polisi 600, pamoja na askari polisi na wanajeshi kutoka Cote d'Ivoire wamepelekwa katika eneo hilo.

Ijumaa usiku, utulivu umekua ukirejea, kwa mujibu wa wakazi. Viongozi katika mji huo wametoa wito kwa utulivu. Ujumbe unaoongozwa na Waziri wa Sheria ambaye ni mzaliwa wa mkoa huo unasubiriwa Jumamosi Machi 26 katika mji wa Bouna.