BURUNDI-RWANDA-DIPLOMASIA

Burundi: Waziri wa zamani wa Rwanda Jacques Bihozagara afariki ghafla

Kifo cha waziri wa zamani wa Rwanda katika gereza la Mpimba mjini Bujumbura, chazua maswali mengi, Machi 30, 2016.
Kifo cha waziri wa zamani wa Rwanda katika gereza la Mpimba mjini Bujumbura, chazua maswali mengi, Machi 30, 2016. © REUTERS/Jean Pierre Aime Harerimama

Waziri wa zamani na mwanadiplomasia wa zamani wa Rwanda Jacques Bihozagara, ambaye alikuwa balozi nchini Ufaransa na Ubelgiji, amefariki ghafla Jumatano hii Machi 30 katika gereza kuu la Mpimba mjini Bujumbura , ambako alikuwa akizuiliwa tangu Desemba 2015.

Matangazo ya kibiashara

Mwanadiplomasia huyo wa zamani wa Rwanda alikua akituhumiwa na utawala wa Nkurunziza kuwa aliingia Burundi kufanya ujasusi.

Vyanzo vya ndani vya gereza kuu la Mpimba vinaeleza wazi: Jacques Bihozagara alikua na hali "nzuri" jana asubuhi. Lakini baadae mchana alihisi hali yake haiko sawa, akachukua uamuzi wa kwenda hospitali ilio ndani ya gereza. Wafungwa wenzake wanahakikisha kuwa "walishangaa" kusikia baada ya dakika ishirini kuwa Waziri huyo wa zamani wa Rwanda amefariki.

Nini kilichotokea katika hospitali hii? Ni sababu ipi ya kifo chake? maswali yote haya yamekosa majibu, wakati ambapo mkurugenzi wa gereza la Mpimba amekataa kujieleza juu ya kifo hicho Jumatano hii Alaasiri.

Balozi wa Rwanda nchini Burundi, Amandin Rugira, amethibitisha taarifa kwenye Twitter, akitangaza kwamba bado hajajua sababu za kifo chake. Afisa mwandamizi kwenye wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda ambaye amewasiliana na RFI amesema wazi. Amehakikisha kwamba Rwanda "ilishtushwa" na taarifa hiyo, huku akibaini kwamba serikali ya Rwanda inaamini kwamba mwanadiplomasia huyo mstaafu alikuwa kizuizini kinyume cha sheria. Na ameongeza : "Tunaomba mamlaka ya Burundi kutoa mwanga juu ya kifo cha ghafla ambacho kiinaibua maswali mengi. "

Bw Bihozagara, alikua akijihusisha na biashara tangu alipostaafu, alikuwa amewekeza nchini Burundi, nchi ambapo alizaliwa na aliishii katika ujana wake, na alikua akiingia nchini humo mara kwa mara kwa ajili ya biashara yake. Alikamatwa Desemba 4, 2015 na Idara ya Ujasusi ya Burundi, ambayo inasimamiwa moja kwa moja na Rais Pierre Nkurunziza. Idara hiyo imekua ikimshtumu "kufanya ujasusi kwa maslahi ya nchi yake" wakati ambapo kunashuhudiwa mdororo wa mahusiano kati ya nchi hizo mbili, kwa sababu ya mgogoro wa kina unaoikabili Burundi kwa sasa.

Kifo cha afisa wa zamani muhimu katika serikali ya Rwanda katika gereza la Burundi kinaweza kukuza uadui zaidi katika mahusiano ambayo tayari yamekwisha ingiliwa na dosari. Tayari katika mitandao ya kijamii, watu wengi wanahitaji kuona msimamo mkali wa Rwanda wakati upande mwengine, wamekua kimya na aibu ikitawala.