DRC-KATUMBI-SIASA

Moïse Katumbi alaani vitisho vya serikali dhidi yake

Moise Katumbi hapa mwezi Novemba 2011 Lubumbashi wakati wa mkutano na wawakilishi wa MONUSCO.
Moise Katumbi hapa mwezi Novemba 2011 Lubumbashi wakati wa mkutano na wawakilishi wa MONUSCO. © AFP / PHIL MOORE

Mkuu wa zamani wa mkoa wa zamani wa Katanga, Moïse Katumbi amelaani vikali kile alichokiita mpango wa serikali wa kutaka kumkatisha tamaa ya kuwania katika uchaguzi wa urais.

Matangazo ya kibiashara

Tamko hilo linakuja saa chache baada ya kuonekana askari polisi wengi wakishirikiana na maafisa wa Idara ya Ujasusi Alhamisi hii asubuhi wakifanya mzunguko wa nenda-rudi karibu na makazi ya mwanasiasa huyo wa upinzani ambaye kwa zaidi ya miaka kumi alikua mshirika wa karibu wa Rais Joseph kabila.

Moïse Katumbi Chapwe anasema vitisho hivyo vimeanza pale tu alipotangaza, Jumatano wiki hii, nia yake ya kuwania katika kinyang'anyiro cha urais mwaka huu. Amebaini kwamba askari polisi na maafisa wa Idara ya Ujasusi walisitisha mzunguko huo baada ya kikosi ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa MONUSCO kuwasili katika makazi yake kutoa ulinzi, ambapo amekaribisha msaada huo wa kikosi hicho.

Wakati huo huo Marekani kupitia ubalozi wake nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imelaani taarifa ya "uongo" iliyotolewa na Waziri wa Sheria wa DR Congo, Alexis Thambwe Mwamba, kwamba kuna baadhi ya askari wa zamani wa Marekani ambao wamekua wakiajiriwa na Moïse Katumbi kama askari mamluki kwa ajili ya kutumiwa kwa maslahi yake binafsi. Marekani imesema raia wake Darryl Lewis ambaye amehusishwa na serikali ya DR congo kuwa ni miongoni mwa mamluki wanaotumiwa na Moïse Katumbi Chapwe ni uzushi mtupu.

"Merryl Lewis ni mfanyakazi wa shirika kutoka Marekani linalohusika na kutoa huduma ya nasaha kwa wateja wake duniani, ambalo kwa sasa linaendesha shughuli yake katika mkoa wa zamani wa Katanga, " Marekani imesema katika taarifa yake.

Jumatano wiki hii, Waziri wa Sheria Alexis Thambwe Mwamba aliomba Ofisi ya mashitaka kuanzisha uchunguzi kuhusu askari mamluki wanaoajiriwa na Moïse Katumbi Chapwe kwa kutumiwa kwa maslahi yake binafsi.

Bw Katumbi Chapwe, kwenye akaunti yake ya Twitter, amesema hababaishwi na vitisho hivyo vya serikali, na bado anashikilia msimamo wake wa kuwania katika kiti cha urais katika uchaguzi wa urais uliyopangwa kufanyika mwaka huu.

Kwa upande wake serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekanusha madai hayo ya mkuu wa zamani wa mkoa wa zamani wa Katanga, ikibaini kwamba ni tuhuma zisizokua na msingi.