DRC-KATUMBI-SIASA

Moïse Katumbi arejea nyumbani baada ya kusikilizwa

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, mkuu wa zamani wa mkoa wa Katanga na mgombea urais Moïse Katumbi amerejea nyumbani Jumatatu hii jioni baada ya kusikilizwa katika Ofisi ya mashitaka ya mkoa wa Lubumbashi.

Moïse Katumbi, Lubumbashi, Mei 28.
Moïse Katumbi, Lubumbashi, Mei 28. © AFP PHOTO / FEDERICO SCOPPA
Matangazo ya kibiashara

Vyombo vya seria vinamshtumu kwamba amekua akiajiri askari mamluki, hasa askari wa zamani wa Marekani. Kesi hii itaendelea Jumatano wiki hii.

Moïse Katumbi tayari amerejea nyumbani. alilakiwa na umati mkubwa wa watu alipoondoka katika Ofisi ya mashitaka ya mkoa wa Lubumbashi . Polisi hata hivyo, imetumia mabomu ya machozi kwa kuwatawanya wafuasi wake, kwa mujibu wa naibu kiongozi wa muungano wa vyama vya upinzani vya G7, moja ya makundi matatu ya vyama vya upinzani linalomuunga mkono mkuu wa zamani wa mkoa wa Katanga.

Bw Katumbi hajashitakiwa, lakini hatua muhimu, hajamaliza kusikilizwa. Kikao hiki kimesimamamishwa na kitaendelea Jumatano asubuhi. "Tumechoka na namna mwendesha mashitaka ameeendelea kusisitiza. Mteja wetu kwa mara nyingine tena amekanusha kabisa tuhuma dhidi yake, " Wakili Kapiamba amesema.

Akihojiwa na RFI, ameongeza kuwa Katumbi yuko sawa, na kwamba "ukweli siku moja utajulikana na itaonekana kwamba ni njama za kumzuia kuwania katika kiti cha urais."

Maafisa wanne wa usalama wa mkuu wa zamani wa mkoa wa Katanga, ikiwa ni pamoja na raia wa Marekani, walikamatwa wiki iliyopita. Kaka wa mmoja wa walinzi hao wa Bw Katumbi amekamatwa Jumatatu hii .

Ubalozi wa Marekani ulisema katika taarifa yake wiki iliyopita kuwa madai ya kuajiri mamluki "yalikua ya uongo" na ulionyesha wasiwasi wake mkubwa.