Zoezi la kutafuta kisanduku cheusi laendelea
Imechapishwa:
Misri inaendelea kutafuta kisanduku cheusi, kinachohifadhi mawasiliano cha ndege yake ya abiria iliyozama katika Bahari ya Mediterranean wiki iliyopita kufahamu ikiwa ilikuwa ni ajali ya kawaida au ilishambuliwa na magaidi.
Misri ilisema siku ya Jumapili kuwa ilituma manowari katika bahari ya Mediterranean, na chombo cha Ufaransa kinatarajiwa Jumatatu hii kuwasili katika eneo hilo ili kushiriki katika zoezi hilo.
Waziri wa Usafiri wa Anga wa Misri alibaini mapema wakati wa ajali ya ndege hiyo kuwa kuna uwezekano ndege hiyo kuwa ilishambuliwa . Lakini tangu wakati huo hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio la ndege hiyo ya shirika la ndege la EgyptAir.
Hata hivyo Rais Abdel Fattah al-Sisi amesema ni mapema sana kubaini hasa chanzo cha kuanguka kwa ndege hiyo.
Ndege hiyo MS804 ilianguka katika Bahari ya Mediterranean usiku wa Jumatano kuamkia Alhamisi juma lililopita ikiwa na watu 66, baada ya kutoweka kwenye mitambo ya rada. Wamisri 30 na Wafaransa 15 ni miongoni mwa abiria waliokuwemo katika ndege hiyo.
Abiria wengine waliokuwemo katika ndege ni pamoja na raia wawili kutoka Iraq, wawili kutoka Canada na raia wa Algeria, Ubelgiji, Uingereza, Chad, Ureno, Saudi Arabia na Sudan.
Wahudumu wa ndege hiyo walikua saba na maafisa 3 wa usalama.
Baadhi ya mabaki ya ndege hiyo yalipatikana mwishoni mwa wiki iliyopita