DRC-PPRD-SIASA

DRC: chama tawala kimefuta maandamano yake

Mkuu wa mkoa wa Kinshasa na baraza lake la mawaziri Jumanne Mei 24. Kulia, mkuu wa polisi katika mji wa Kinshasa, jenerali Kanyama.
Mkuu wa mkoa wa Kinshasa na baraza lake la mawaziri Jumanne Mei 24. Kulia, mkuu wa polisi katika mji wa Kinshasa, jenerali Kanyama. © RFI/Sonia Rolley

Maandamano ya upinzani yatafanyika bila shaka Alhamisi hii Mei 26 katika mji wa Kinshasa na katika baadhi ya mikoa kama vile Kivu Kaskazini. Moja ya miungano mitatu ya upinzani, Front Citoyen, umeendelea kushikilia msimamo wake wa kuandamana licha ya kupigwa marufuku na viongozi.

Matangazo ya kibiashara

Upinzani umetoa wito wa kufanyika uchaguzi ndani ya muda wa uliopangwa kikatiba na kulaani mauaji katika wilaya ya Beni.

PPRD, chama tawala, ambacho kilikua pia kimetoa wito wa kufanyika kwa maandamano kwa siku kadhaa kuanzia Jumatano wiki hii, kimeahirisha maandamano yake. Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito kwa pande zote kujizuia na machafuko au uhasama wowote.

Chama tawala kimeamua kufuta maandamano kiliyokua kimepanga kufanya kuanzia Jumatano wiki hii kwa ombi la mkuu wa mkoa wa Kinshasa. Katika mkutano wa kisiasa uliyofanyika kwenye makao makuu ya chama cha PPRD katika mtaa wa Limité, balozi Mova alitoa taarifa kwa wafuasi wa chama hicho, akisema kuwa uamuzi huo umechukuliwa kwa kuepusha vurugu. hata hivyo Katibu mkuu wa chama cha PPRD ameushtumu upinzani kuchukua uamuzi wa kufanya maandamano kwa terehe ambayo chama tawala kilikua kimepanga kufanya maandamano yake mjini Kinshasa.

Upinzani, kwa upande wake umeendelea kushikilia msimamo wake wa kuandamana nchini kote, ikiwa ni pamoja na katika mji wa Kinshasa na katika miji yote ambapo wamekuwa wamepigwa marufuku, hasa katika miji ya Mbuji Mayi, Lubumbashi, Bunia na Goma. Katika mji wa Goma, upinzani ulitoa taarifa ya kukamatwa Jumatano wiki hii wawakilishi wake wawili, mmoja kutoka UNC na na mwengine Ecide. Wote wawili wameachiliwa. Katika mji wa Matadi, katika mkoa wa Bas-Congo, hata hivyo wanasiasa saba wa upinzani waliokamatwa wakati wa mkutano wa maandalizi ya maandamano bado wanashitakiwa kwa kuchochea vurugu.

Umoja wa Mataifa watoa onyo

Kwa upande wake, Afisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imetoa onyo kwa serikali ya Congo, ikiwataka viongozi wa nchi hiyo kuhakikisha kila mtu anapewa haki ya kufanya maandamano kwa uhuru na amani.