BURUNDI

Umoja wa Mataifa kutoongeza muda kwa polisi wa Burundi chini Afrika ya Kati

Polisi wa Burundi wakiwa katika doria mjini Bangui
Polisi wa Burundi wakiwa katika doria mjini Bangui REUTERS/Alain Amontchi

Umoja wa Mataifa unahitimisha mara moja huduma ya vitengo vya polisi kutoka Burundi katika ujumbe wake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa sababu ya ushiriki wao katika ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi zao, maafisa wamesema jana Ijumaa.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema uamuzi wa kutotafuta mbadala wa kikosi cha Burundi wakati muda wake wa huduma utakapomalizika, umeamuliwa kwenye makao makuu ya umoja huo kufuatia hali ya mambo ilivyo kwa sasa nchini Burundi

Stefan Feller, mshauri wa juu wa polisi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, amesema uamuzi huo ulitolewa kutokana na madai ya sasa ya ukiukwaji mkubwa unaoendelea wa haki za binadamu nchini Burundi.

Umoja wa Mataifa umekitaarifu rasmi kikosi cha Burundi mjini New York kuhusu uamuzi huo.

Shirika lisilo la kiserikali la nchini Burundi FOCODE mwezi Februari liliuomba Umoja wa Mataifa kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu unayofanywa na polisi wa Burundi ambao kwa sasa wanahudumu mjini Bangui.

Kwa mujibu wa FOCODE, Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amewatunuku kazi katika vikosi vya Umoja wa mataifa wanajeshi na polisi ambao kwa kiasi kikubwa walihusika katika ukandamizaji wa wapinzani wake wa kisiasa.