KENYA

Upinzani nchini Kenya kuendelea na maandamano ya kila Jumatatu

REUTERS

Mkuu wa jeshi la polisi nchini Kenya, Josephu Boinett, ametoa onyo kali kwa viongozi wa muungano wa upinzani wa Cord dhidi ya maandamano yao waliyoapanga kuyafanya siku ya Jumatatu, June 6, wakipinga kuendelea kuwepo madarakani kwa makamishna wa tume ya uchaguzi nchini humo IEBC.

Matangazo ya kibiashara

Onyo la mkuu wa jeshi la polisi linatolewa wakati huu ambapo viongozi hao wa upinzani wakishikilia msimamo wao kuwa maandamano ya kila Jumatatu yatafanyika kama kawaida kwakuwa hakutakuwa na mazungumzo ya kupata muafaka kati yao na Serikali.

Akizungumza kwenye kituo kimoja cha polisi cha Diani, Boinett amesema kuwa maandamano hayo hayana uhalali kisheria na kwamba wale wote watakaokaidi amri ya kutoandamana watakabiliana na nguvu ya sheria.

Mkuu huyo wa polisi ameongeza kuwa jeshi lake lina taarifa moja tu ya uamuzi wa mahakama kuu iliyoutoa awali na kuruhusu muungano wa Cord kufanya maandamano yao June 1, kwenye bustani ya Uhuru na sio kuhusu maandamano yao.

"Wajibu wetu ni kutekeleza sheria za nchi kama zilivyo, na kwamba wakikaidi sheria na kwenda barabarani, sisi, jeshi la polisi tutafanya kile tunachotakiwa kukifanya", alisema Boinett.

Kinara wa muungano wa upinzani, Raila Odinga akihutubia moja ya mikutano yake ya hivi karibuni jijini Nairobi
Kinara wa muungano wa upinzani, Raila Odinga akihutubia moja ya mikutano yake ya hivi karibuni jijini Nairobi REUTERS/Goran Tomasevic

Haya yanajiri wakati huu ambapo mkuu huyo wa jeshi la polisi anakabiliwa na changamoto ya usalama hafifu kwenye kaunti ya Kwale, ambapo hivi karibuni maofisa watatu kwenye kambi ya nyumbu waliuawa kwenye kijiji cha Bongwe, Msambweni, ambapo polisi inaamini shambulio hilo lilitekelezwa na wapiganaji wa Al-Shabab.

Juma moja lililopita muungano wa upinzani wa Cord ulitangaza kusitisha kwa muda maandamano yao ya kila Jumatatu nchi nzima kupinga makamishna wa tume ya IEBC kuendelea kusalia madarakani, na walifanya hivyo kutoa mwanya wa kufanyika mazungumzo.

Mwishoni mwa juma wakati wa maombi maalumu ya kitaifa, rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, walikanusha kufikia makubaliano katikati ya juma lililopita na kinara wa Cord Raila Odinga wakati walipomwalika Ikulu ya Nairobi.

Naibu wa rais Ruto, amesema kamwe hawakukubaliana lakini waliafikiana kuwa Cord ifuate sheria inaposhinikiza maofisa wa IEBC kuondoka madarakani, kauli ambayo imeonekana kuwakera viongozi wa upinzani ambao wametangaza kurejea Jumatatu hii.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto REUTERS/Noor Khamis

Rais Kenyatta kwa upande wake amewaonya viongozi hao na kuwataka waheshimu katiba, huku akiongeza kuwa vyombo vya usalama habitamfumbia macho mtu yeyote atakayehatarisha usalama kwenye maandamano yao ambayo amesema haya tija wala msingi wowote kwakuwa mihimili ya sheria ipo.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wameonya kuhusu kutofikiwa muafaka kati ya Cord na Serikali kuhusu tume ya IEBC, huku wakidai kuwa nchi hiyo iko hatarani kutumbukia kwenye machafuko mengine wakati wa uchaguzi ikiwa muafaka kati ya pande hizo mbili hautapatikana.

Viongozi wa dini walionesha matumaini yao kuhusu uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo ya pande mbili zinazokinzana, na hasa baada ya upinzani kutangaza kusitisha maandamano yao kwa juma moja kupisha kuanzishwa kwa mchakato wa mazungumzo hayo, jambo ambalo sasa linaonekana ni wazi juhudi zao zinaelekea ukingoni.

Kinara wa Cord, Raila Odinga tayari alikuwa ameshatangaza timu ya wafuasi wao watakaoshiriki kwenye mazungumzo na kutoa makataa ya hadi kufikia Jumapili hii upande wa Serikali nao uwe umetangaza timu yao ama sivyo watarejea barabarani.