KENYA-SOMALIA

Kenya na Somalia washindwa kuelewana kuhusu suala la wakimbizi

Kambi ya wakimbizi wa Kisomali ya Dadaab, kaskazini mwa kenya.
Kambi ya wakimbizi wa Kisomali ya Dadaab, kaskazini mwa kenya. © Natasha Lewer / MSF

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamoud, wameshindwa kukubaliana kuhusu mpango wa serikali ya Nairobi kuanza kuwarejesha nyumbani maelfu ya wakimbizi wa Somalia wanaopatiwa hifadhi kwenye kambi ya Daadab.

Matangazo ya kibiashara

Katika mazungumzo yao baada ya kukutana kwenye ikulu ya Nairobi, rais Kenyatta alisisitiza msimamo wa nchi yake kuhusu kuwarejesha nyumbani kwa wakayi wakimbizi hao, huku rais wa Somalia, Sheikh Mohamoud, akitaka zoezi hilo lifanyike kwa wakimbizi ambao wako tayari kurejea nyumbani kwa hiari.

Rais Kenyatta, amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na utawala wa Mogadishu, katika kuhakikisha kunakuwa na utaratibu mzuri ambao utatumiwa kuwarudisha wakimbizi hao bila kutumia nguvu.

Juma hili rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamoud, alifanya ziara katika kambi ya Daadab na kukutana na raia kutoka nchini mwake na kuwaahidi kuendelea kuwahudumia na kuishawishi Serikali kutowarudisha kwa nguvu nyumbani, mpango ambao umekosolewa na jumuiya ya kimataifa.