TANZANIA

Upinzani wakosoa Polisi kukataza mikutano ya kisiasa

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe Tumaini Makene/ Chadema

Upinzani nchini Tanzania umekosoa hatua ya jeshi la polisi nchini humo kupiga marufuku maandamano na mikutano ya vyama vya siasa kwa kile jeshi hilo linasema ni kwasababu za kiusalama.

Matangazo ya kibiashara

Upinzani unasema kuwa hatua ya jeshi la polisi kupiga marufuku kufanyika kwa mikutano yoyote ya kisiasam inalenga kuminya demokrasia na uhuru wa watu kutoa maoni yao na kuikosoa Serikali.

Akizungumza akiwa mjini Mwanza, Tanzania, mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzaniam CHADEMAm Freeman Mbowe, amesema wamesikitishwa na tangazo la polisi ambalo amesema ni wazi liliwalenga wao.

Mbowe amesema kuwa wao kama chama wamesikitishwa na hatua ya jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, ambalo hapo jana lilitumia nguvu kuwatawanya maelfu ya wafuasi wa chama hicho waliokuwa tayari kuwasikiliza viongozi wao.

Upinzani unasema kuwa, kupiga marufuku kufanyika kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa kunarudisha nyuma harakati za kuimarisha demokrasia nchini Tanzania, na kwamba Serikali inalenga kurejesha mfumo wa chama kimoja madarakani.

Mwenyekiti huyo akaongeza kuwa, wao kama chama wataketi kutathmini tangazo hili la jeshi la polisi, na kutangaza hatua zaidi za kuchukua ikiwa watakaidi agizo hili la polisi au la.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa ikiwa kama kweli polisi wamepata taarifa za kiintelijensia kuwa huenda mikutano hiyo ingekumbwa na vurugu, basi wana haki ya kuipiga marufuku lakini vinginevyo watakuwa wameenda kinyume na katiba ya nchi inayotoa uhuru wa watu kukusanyika na kutoa maoni yao bila kuingiliwa.

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kupitia mtandao wake wa kijamii, ameendelea kuikosoa Serikali kwa kutaka kuminya demokrasia ndani na nje ya bunge, na kwamba kukataza kufanyika kwa mikutano ya hadhara ni wazi inalenga kuzuia watu kuikosoa Serikali.

Siku ya Jumanne jeshi la polisi nchini Tanzania kupitia kwa kamishna wa operesheni na mafunzom alitangaza kusitishwa kwa maandamano na mikutano ya kisiasa kwa kile alichosema wanazotaarifa kuwa ikiwa itaendelea itatatiza hali ya usalama ikiwemo mivutano kati ya wafuasi wa pande mbili za kisiasa.