LIBYA-IS

Mapigano yarindima Sirte

Mji wa sirte umekumbwa na mapigano kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa kundi la Islamic State.
Mji wa sirte umekumbwa na mapigano kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa kundi la Islamic State. REUTERS/Anis Mili

Mapambano kuuchukua mji wa Sirte nchini Libya kutoka kwenye mikono ya wapiganaji wa kiislamu wa Islamic State, yameshika kasi, baada ya hapo jana vikosi vya serikali ya umoja wa kitaifa kuelekeza mashambilizi zaidi kwenye mji huo.

Matangazo ya kibiashara

Wataalamu wa masuala ya vita wanabashiri kuwa mji wa Sirte huenda ukawa chini ya umiliki wa serikali ya kitaifa ndani ya siku chache zijazo hasa baada ya vikosi hivi kuongeza nguvu kuwakabili wanajihadi hao.

Serikali ya Marekani imekaribisha kwa mikono miwili operesheni hii ya kujaribu kuingia katikati mwa mji wa Sirte, mji ambao ndiko alikozaliwa aliyekuwa rais wa taifa hilo marehemu kanali, Muamar Gaddafi.

Wapiganaji hasimu ambao walikuwa wanajaribu kuuchukua mji huo bila mafanikio, wameonesha kukubali usaidizi wa vikosi vya Serikali ya kitaifa, uamuzi ambao unaonesha kuwa ikiwa watafanikiwa kuuchukua mji huo, itakuwa pigo kubwa kwa wapiganaji wa kundi la Islamic State ambao waliufanya kuwa ngome yao.

Nchi washirika zinazosaidia kusaka suluhu ya kudumu nchini Libya, zinafikiri namna ya kuvisaidia vikosi hivyo kuwakabilia wapiganaji wa Islamic State na pengine kuuchukua mapema zaidi mji huo.