OSCAR PISTORIUS

Mtaalamu: Pistorius hana uwezo wa kutoa ushahidi kwa sasa

Mwanariadha mwenye ulemabu, Oscar Pistorius, akiwa mahakamani kusikiliza kesi yake 13 june 2016
Mwanariadha mwenye ulemabu, Oscar Pistorius, akiwa mahakamani kusikiliza kesi yake 13 june 2016 REUTERS/Phill Magakoe/Pool

Kesi dhidi ya mwanariadha mwenye ulemavu raia wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius, imeanza kusikilizwa tena Jumatatu ya wiki hii ambapo mahakama itaamua kuhusu adhabu mpya anayopaswa kupewa mwanariadha huyo. 

Matangazo ya kibiashara

Awali mahakama kuu ilikuwa imemuhukumu kifungo cha miaka 5 jela kwa kosa la kumuua bila kukusudia mchumba wake, Reeva Steenkamp, miaka mitatu iliyopita, ambapo aliachiwa huru mwaka uliopita baada ya kutumikia robo tatu ya kifungo chake jela.

Hata hivyo upande wa mwendesha mashtaka wa Serikali, ulikata rufaa kupinga hukumu ya awali iliyotolewa na jaji Thokozile Masipa, ambaye aliagiza mwanariadha huyo kwenda jela kwa miaka 5.

Pistorius, alimuua mchumba wake Reeva Steenkamp, mwanamitindo na mwanafunzi wa sheria, alfajiri ya siku ya wapendanao mwaka 2013, akidai kuwa alidhani ni wezi walikuwa wamevamia nyumbani kwake.

Mwanariadha huyo aliwasili kwenye mahakama ya Gauteng akiambatana na familia yake, ambapo muda wote wakati kesi ikiendelea alionekana kuinamisha kichwa chake chini akilengwalengwa na machozi.

Daktari wa Oscar Pistoriu aliyemtibu matatizo ya msongo wa mawazo kuanzia kwenye kesi ya awali, amesema kuwa, kama ingekuwa ni amri yake, basi angeagiza mwanariadha huyo kuwekwa chini ya uangalizi maalumu kwakuwa kwa sasa hana uwezo wa kutoa ushahidi muhimu kutokana na kukabiliwa na msongo wa mawazo.

Mwanasaikolojia anayemtibu, Pistorius, Jonathan Scholtz ameiambia mahakama kuwa mteja wake anadalili zote za mtu mwenye msongo mkubwa wa mawazo ambao unamsababishia kutokuwa na kumbukumbu muhimu na hata ujibu wa maswali yake umekuwa si wa kuridhisha.

Jonathan Scholtz, ameongeza kuwa kwasasa mteja wake hawezi kutoa ushahidi wowote kuhusiana na kesi inayoendelea, na kwamba amekata tamaa ya kuendelea na kesi yake.

Siku ya mwisho ya kusikilizwa kesi ya Oscar Pistorius, ambapo Mwendesha mashataka aliomba kifungo cha miaka 10 dhidi ya mwanariadha huyo mlemavu, Oktoba 17 mwaka 2014.
Siku ya mwisho ya kusikilizwa kesi ya Oscar Pistorius, ambapo Mwendesha mashataka aliomba kifungo cha miaka 10 dhidi ya mwanariadha huyo mlemavu, Oktoba 17 mwaka 2014. REUTERS/Werner Beukes/Pool

Mwendesha mashtaka wa Serikali anataka mwanariadha huyo ahukumiwe upya, kwakuwa uamuzi wa awali ulitafsiriwa vibaya kisheria, na kwamba wanataka ahukumiwe kwa kosa la kuua kwa kukusudia jambo ambalo upande wa utetezi unapinga.

Jaji aliyesikiliza kesi ya awali na kuitolea uamuzi, Thokozile Masipa, ndiye jaji ambaye safari hii atatoa hukumu nyingine dhidi ya mwanariadha huyo baada ya kusikiliza pande zote mbili.

Ikiwa mahakama itajiridhisha na kutoa hukumu mpya, Oscar Pistorius huenda akakabiliwa na adhabu ya kifungo cha miaka 15 jela kwa kosa la mauaji, na huenda ikapungua baada ya kuwa ameshatumikia sehemu ya kifungo cha awali.

Wazazi wa Steenkamp, walikuwepo mahakamani na baba yake, Barry anaweza kupanda kizimbani kama shahidi, ambapo anatarajiwa kuiomba mahakama kutoa adhabu kubwa zaidi ya ile ya awali dhidi ya mwanariadha huyo.