KENYA

ODM waitaka Serikali kumkamata Kuria ndani ya saa 24

Raila Odinga, kinara wa muungano wa upinzani nchini Kenya, Cord
Raila Odinga, kinara wa muungano wa upinzani nchini Kenya, Cord REUTERS/Noor Khamis

Chama cha upinzani nchini Kenya ODM kimeshutumu vikali matamshi ya mbunge, Moses Kuria, aliyenukuliwa akidai kuwa atapanga njama za kuuawa kwa waziri mkuu wa zamani na kinara wa muungano wa Cord, Raila Odinga. 

Matangazo ya kibiashara

Wabunge wa upinzani wamesema kuwa, wanatoa saa 24 kwa mkuu wa jeshi la Polisi nchini humo, Joseph Boinnet,kumkamata mbunge huyo, na wengine wawili wanaotaka kabila la Waluo kuondoka katika mji wa Nakuru, ambao ni ngome ya chama tawala Jubilee.

Wakizungumza na wanahabari jijini Nairobi, wabunge wa ODM wamesema matamshi ya mbunge huyo yanaonesha nia mbaya dhidi ya kiongozi wao na kuonya kuwa matamshi kama haya hayavumililiki na kukubalika katika nchi hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya wenzakwe, mbunge wa upinzani, Aisha Jumwa, amesema ikiwa polisi haitachukua hatua na kuwakamata wabunge hao, wafuasi wa upinzani watachukua hatua na kuanza kujilinda dhidi ya wanasiasa kama Kuria.

“Sisi ni wakenya na tuna haki ya kuishi popote hapa nchini, tumempa Inspekta wa polisi saa 24 kuchukua hatua, la sivvyo serikali ifahamu kuwa Mheshimiwa Raila Odinga ana wafuasi ambao wanaweza kupanga lao ikiwa hawatakamatwa,” Bi Jumwa alisisitiza.

Mbali na chama cha ODM, Mwenyekiti wa Tume ya taifa ya uwiano na utengamano Francis Ole Kaparo amesema kuwa wabunge hao wameagizwa kufika mbele ya Tume hiyo ili kuhojiwa baada ya kutoa matamshi ya kichochezi.

“Nimemwagiza Mbunge wa Bahati na Nakuru Mjini kufika mbele ya tume hii siku ya Alhamisi au Ijumaa, lakini pia Bwana Kuria kufika,”

“Huyu Kuria, tumekuwa tukiiomba Mahakama iondowe dhamana iliyompa kutokana na matamshi aliyotoa hapo awali, lakini Mahakama imekataa kutupa sikio,” alisisitiza Kaparo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Odinga alikuwa na mkutano wa hadhara mjini Nakuru lakini vijana kutoka chama kilichoko madarakani Jubilee walijaribu kumzuia kutohutubia kabla ya polisi kutumia nguvu kuwasambaratisha.

Hii sio mara kwanza kwa Moses Kuria kutoa matamshi ya uchochezi dhidi ya Odinga, na matamshi yake ya hivi karibuni yanaonekana kuzua hali ya wasiwasi kuelekea uchaguzi Mkuu mwaka ujao.

Mwaka 2007, matamshi kama haya yalisababisha mapigano ya kikabila nchini humo baada ya kumalizika kwa uchaguzi a urais na kusababisha zaidi ya watu 1,300 kufariki.