UN

UN: Tukomeshe ukatili dhidi ya watu wenye Ualbino

Mtoto mwenye Ualbino ambaye alinusurika kuuawa nchini Tanzania, akiwa hospitalini
Mtoto mwenye Ualbino ambaye alinusurika kuuawa nchini Tanzania, akiwa hospitalini Under the same Sun

Tarehe 13 Juni kila mwaka dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya uelewa kuhusu watu wenye Albino, lakini siku hii inaadhimishwa huku matukio ya unyanyapaa na ukatili dhidi yao vikiongezeka barani Afrika. 

Matangazo ya kibiashara

Siku hii inaadhimishwa wakati ambapo licha ya maazimio mbalimbali yaliyopitishwa nyombo vya kutunga sheria vya ndani ya nchi na vile vya kimataifa, bado mauaji ya watu wenye Ualbino yameendelea kukithiri.

Vyombo vyote viwili vya kimataifa, umoja wa Afrika AU na umoja wa Mataifa, vimepitisha maazimio maalumu yanayowalinda watu wenye Ualbino pamoja na kuzitaka nchi wanachama za umoja huo, kupitisha sheria kali kupitia mabunge yao, kuwashughulikia wahalifu wanaojihusisha na mauji ya Albino.

Mtu mwenye Ualbino akiwa hospitalini akipatiwa matibabu baada ya sehemu ya mkono wake kukatwa, Tanzania
Mtu mwenye Ualbino akiwa hospitalini akipatiwa matibabu baada ya sehemu ya mkono wake kukatwa, Tanzania Under the same Sun

Umoja wa Mataifa kupitia baraza lake la tume ya haki za binadamu, ilipitisha azimio mwaka 2013 ikitaka watu wenye Ualbino walindwe na kuepuka vitendo vya unyanyapaa dhidi yao. Zaidi azimio hili katika kujibu wito uliokuwa unatolewa na mashirika ya kiraia kutambua kwa umuhimu wake kundi la watu wenye Ualbino na kutoa mahitaji maalumu, tarehe 26 March 2015, baraza hilo liliunda kamati maalumu na kuipa uwezo wa kuwa jopo huru kuchunguza na kupendekeza hatua za kuchukua dhidi ya vitendo vyovyote vinavyowahusu watu wenye ulemavu na Ualbino.

Wakati dunia inapoaadhimisha siku hii, ni juma moja tu limepita ambapo nchini Malawi, mtu mmoja mwenye Ualbino aliuawa na watu wasiofahamika, tukio ambalo sasa linafanya idadi ya watu wenye Ualbino waliouawa nchini Malawi, kufikia watu 18.

Mashirika ya kiraia nchini Malawi, May 25 mwaka huu yaliipa Serikali ya Malawi siku 21 kuwa imepitisha muswada wa sheria inayowalinda watu wenye Ualbino ama sivyo wangeandaa maandamano ya nchi nzima kushinikiza wabunge kuiunga mkono sheria hiyo.

Wasamaria wema wakiwasaidia kula, watoto wenye Ualbino ambao sehemu ya viungo vyao imekatwa, Tanzania
Wasamaria wema wakiwasaidia kula, watoto wenye Ualbino ambao sehemu ya viungo vyao imekatwa, Tanzania Under the same Sun

Hivi karibuni rais wa Malawi, Peter Wamutharika, alizungumza na vyombo vya habari na kueleza masikitiko yake kutokana na nchi yake kuendelea kushuhudia mauaji ya watu wenye Ualbino, matukio ambayo amesema hayakubaliki na Serikali yake inafanya kila linalowezekana kukomesha mauaji hayo.

Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Malawi, wanailaumu Serikali kwa kushindwa kuwakamata na kuwahukumu kwa wakati watu wanaokamatwa wakiwa na viungo vya binadamu kwa lengo la kuviuza, na badala yake kesi dhidi ya watuhumiwa zimekuwa zikichukua muda.

Hivi karibuni watuhumiwa wanne walihukumiwa na mahakama kutumikia kifungo cha maisha na wengine miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na biashara ya viungo vya watu wenye Ualbino.

Kuanzia mwaka 2000, nchini Tanzania pia vitendo hivi vilikithiri na hasa nyakati za kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, ambapo matukio kadhaa ya watu kuuawa na kujeruhiwa kwa imani za kishirikina yaliripotiwa.

Bunge la nchi hiyo limepitisha sheria ya kuwalinda watu wenye ulemavu, sheria ambayo hata hivyo wanaharakati wa haki za binadamu licha ya kupongeza bado wanaoza inamapungufu, kwakuwa matukio ya kuuawa watu wenye Ualbino yameendelea kuripotiwa.

Mmoja wa watu wenye Ualbino nchini Tanzania
Mmoja wa watu wenye Ualbino nchini Tanzania Under the same Sun

Tangu mwaka 2000, kumeripotiwa mashambulizi dhidi ya watu wenye Ualbino zaidi ya 448 katika nchi 25 barani Afrika, ambapo vifo vilivyorekodiwa ni 172 na matukio 276 ya watu hao kujeruhiwa lakini sehemu ya viungo vya mwili kuondolewa.

Ripoti nyingi zimeonesha kuwa watu wenye Ualbino wanauawa kwasababu za imani za kishirikina kwa baadhi ya watu kuamini kuwa viungo vyao vinaweza kuwaletea utajiri, jambo ambalo haliko sahihi zaidi ya kukiuka haki za binadamu.

Baadhi ya matukio dhidi ya watu wenye Ualbino, yanahusisha ukataji wa viungo vya mwili, ukatili dhidi yao, kubakwa na majaribio ya utekaji nyara.

Baadhi ya mashirika yanayotetea watu wenye Ualbino yanasema takwimu hizi ni sehemu tu ya matukio ambayol yameripotiwa na kwamba kuna visa vingi ambavyo havijaripotiwa.

Rfikiswahili, inapenda kutumia siku hii, kuikumbusha jamii kuwa watu wenye Ualbino ni kama binadamu wengine na kwamba imani kuhusu kupata utajiri kupitia wao ni suala lisilokubalika na kila mtu anapaswa kuwa mlinzi na kuripoti njama za watu wanaotaka kuwashambulia.