AFRIKA

Wakuu wa nchi za AU, kuanza kuwa na pasi moja ya kusafiria

Nembo ya umoja wa Afrika, AU.
Nembo ya umoja wa Afrika, AU. www.au.int/

Umoja wa Afrika, AU, unajiandaa kuzindua rasmi pasi za kusafiria za kielekroniki "e-Passport", wakati wa mkutano ujao wa 27 wa wakuu wa nchi za Afrika, unaotarajiwa kufanyika jijini Kigali, mwezi Julai mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Mradi huu, ni wa kwanza kukubaliwa toka ulipoidhinishwa mwaka 2014, na unaenda sambamba na malengo ya mwaka 2063 ya umoja wa Afrika ukiwa na lengo la kurahisisha uhuru wa watu kutoka nchi moja kwenda nyingine, bidhaa na huduma kutoka nchi moja na kwenda nyingine kwa lengo la kuimarisha biashara za ndani ya bara la Afrika.

Mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini Zuma, ameelezea hatua hii kama ishara na nembo muhimu kwa bara hili, akisisitiza kuwa ni hatua kubwa ya kuelekea kufikia malengo ya kutengeneza Afrika yenye nguvu.

Dlamini Zuma amesema kuwa lengo namba 2 na namba 7 la malengo ya mwaka 2063 ya umoja wa Afrika, yanasisitiza umoja na mshikamano, sambamba na kuwa na pasi ya pamoja ya kusafiria.

Kundi la kwanza litakalonufaika na mradi huu, utawahusisha wakuu wa nchi, mawaziri wa mambo ya nje na wawakilishi wa kudumu wa umoja wa Afrika kwenye nchi husika na hasa walioko kwenye makao makuu ya umoja huo, mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Umoja wa Afrika unasema pasi hizo zitatolewa wakati wa mkutano wa 27 wa wakuu wa nchi za Afrika, mwezi Julai mwaka huu jijini Kigali, na kuwataka wahusika kuheshimu kuja na nyaraka muhimu zitakazohitajika kwaajili ya kuwezesha kupewa pasi hizo.

Wazo la kutokuwa na vizuizi vya watu kuingia na kutoka nchi moja kwenda nyingine, sio jambo jipya, kwakuwa limeshawahi kuzungumzwa kwenye makubaliano ya Lagos na mkataba wa Abuja.

Nchi za Seychelles, Mauritius, Rwanda, and Ghana tayari zimeshachukua hatua muhimu kurahisisha muingiliano wa watu kwa uhuru ikiwa ni pamoja na kuruhusu biashra ya nchi na nchi kwa kupunguza kiwango cha kupata visa.

Wananchi wote wa bara la Afrika, wanatarajiwa kuwa wanamiliki pasi hizi za kusafiria ifikapo mwaka 2020.