TANZANIA

Upinzani walia demokrasia kuminywa Tanzania

Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini Tanzania, ambao wamelalamika demokrasia kuminywa
Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini Tanzania, ambao wamelalamika demokrasia kuminywa RFI

Vyama vya upijnzani nchini Tanzania vimeilalamikia Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli kwa kuminya demokrasia nchini humo na hata kudhoofisha upinzani ndani na nje ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Matangazo ya kibiashara

Upinzani unadai kuwa demokrasia inaminywa kwa serikali kutumia vyombo vyake vya usalama kuzuia mikutano na makongamano ya kisiasa kinyume na katiba kwa kuwa uhuru wa kukusanyika umeainishwa kwenye kikatiba.

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe amesema kuwa jeshi la polisi linapaswa kufanya kazi kwa kufuata taratibu za kisheria na kutenda haki kwa watu wote na kuepuka kutumika kisiasa.

Kauli hiyo ya Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini imekuja siku chache baada ya jeshi la Polisi kuzuia kongamano la bajeti lililokua limeandaliwa na ACT-Wazalendo kwa ajili ya kujadili bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017.

Amesema hatua ya kuzuia mikutano ya hata ndani ya vyama vya siasa inaharibu nchi na kuminya uhuru wa demokrasia kwa kutumia ubabe jambo ambalo upinzani wameapa kupambana nalo ili demokrasia iweze kuheshimika.

Kabwe alisema kuwa wabunge wa upinzani kamwe hawataogopa kutetea demokrasia ambayo inaelekea kuminywa na hata ikibidi watakua tayari kufungwa jela kwa kutetea maslahi na hai za wananchi.

Zitto amekaririwa na vyombo vya habari nchini Tanzania akifahamisha kuwa sheria namba 5 ya mwaka 1992 inaruhusu na kutoa uhuru kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake bila kuomba kibali polisi bali wanapaswa kutoa taarifa kwa jeshi hilo ili wapatiwe ulinzi.

Kwa upande wake mwanasiasa mkongwe aliyekua mwenyekiti wa Chama cha Wananchi-CUF Profesa Ibrahim Lipumba alisema kuwa demokrasia ikichezewa na Serikali nchi inaweza kuyumba na kupoteza mwelekeo.

Kauli ya Profesa Lipumba imekuja wakati akiwasilisha barua ya kuomba kurejeshwa katika nafasi yake ya uenyekiti wa CUF baada ya kutangaza kujiuzulu mwaka jana wakati wa vuguvugu la uchaguzi.

Lipumba alisema kuwa nchi lazima iendeshwe kwa misingi ya demokrasia ambayo itapatikana kwa umoja wa Watanzania wenyewe na kuepuka siasa zinazominya demokrasia suala ambalo linastahili kupigwa vita na vyama vyote.

Amesema kuwa ameomba kurudi katika nafasi ya uenyekiti ili ashirikiane na wanachama wa CUF kujenga upya demokrasia ambayo iko hatarini kuminywa na serikali ya awamu ya tano ya serikali ya CCM.

Serikali kupitia jeshi la Polisi nchini Tanzania ilipiga marufuku maandamano na mikutano ya kisiasa kutokana na sababu za kiusalama kwa sasa hatua ambayo upinzani umekuwa ukipinga.