UCHAMBUZI - DRC

Kodjo: Muafaka utapatikana kuhusu DRC

Edem Kodjo akihojiwa na RFI jana tarehe 14 juin 2016.
Edem Kodjo akihojiwa na RFI jana tarehe 14 juin 2016. RFI/Sonia Rolley

Mpatanishi wa mzozo wa nchi ya DRC inayojiandaa kufanya uchaguzi wake mkuu mwezi November mwaka huu, amesema kuna matarajio makubwa ya mvutano wa kisiasa uliopo kupatiwa ufumbuzi.  

Matangazo ya kibiashara

Majuma mawili yaliyopita dalili za kuwepo kwa mazungumzo ya kitaifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo zilikua kama zimetoweka, hasa baada ya Mpatanishi wa mazungumzo hayo, Edem Kodjo kuondoka ghafla nchini humo na kuelekea makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU).

Baadhi ya wapinzani wa mrengo wa kati wamemzungumzia Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Togo kuwa na upendeleo kwa chama cha upinzani cha UDPS cha Etienne Tshisekedi, kufuatia kukipa chama hicho jukumu la kuandaa orodha ya washiriki wa kamati ya maandali kwa upande wa upinzani.

Etienne Tshisekedi, kinara wa upinzani nchini DRC
Etienne Tshisekedi, kinara wa upinzani nchini DRC JUNIOR KANNAH / AFP

Hata hivyo, mpatanishi huyo amekabiliwa na upinzani ulio na msimamo mkali kwa kutuhumiwa kuegemea upande wa vyama vinavyomuunga mkono rais Joseph kabila, ambaye anasadikiwa kutaka kutumia mwanya wa mazungumzo hayo kujiongezea muda wa kuendelea kubaki madarakani kinyume na katiba ya Congo.

Wakati hayo yakiendelea, mkutano wa viongozi wa upinzani jijini Brussels tarehe 8 na 9 mwezi huu katika kitongoji cha Genval nchini Ubelgiji ukaja na maazimio kadhaa ambayo yanamtaka mpatanishi Kodjo, kusimamia mazungumzo yatakayoitishwa na Jumuiya ya kimataifa kwa mujibu wa azimio namba 2277 la Umoja wa Mataifa na sio yaliyoitishwa na rais Joseph Kabila.

Kwa hatua iliyofikiwa katika majadiliano ya awali, dalili za kufanyika kwa mazungumzo hayo zinaendelea kudidimia kwa vile upinzani katika muungano wao unaojulikana kwa jina la “Rassemblement” umeweka masharti ambayo kimsingi wanamtaka rais Kabila kuachia ngazi ifikapo mwezi Desemba atakapomaliza muhula wake.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila Oktoba mwaka jana katika mji wa Beni.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila Oktoba mwaka jana katika mji wa Beni. © AFP PHOTO/ALAIN WANDIMOYI

Pamoja na mkanganyiko uliopo, mpatanishi hajakatishwa tamaa kwa vile amekiri kuwa zipo jitihada zilizofanywa licha ya kuwa muda unaendelea kuyoyoma na kwamba mkutano wa Brussels haujapinga kuwepo kwa mazungumzo.

Hapo jana, Edem Kodjo amebainisha kuwa sharti la Upinzani la kutaka kushirikisha jopo la kimataifa ambalo litaundwa na Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Umoja wa mataifa, Jumuiya ya Francophonie, Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADEC na Jumuiya ya nchi za maziwa makuu ICGLR halina pingamizi pamoja na kwamba hapatakuwepo na ushiriki wa nchi moja moja.

Duru za kidiplomasia zinabaini kuwa serikali ya DRC haitaki baadhi ya nchi kushiriki katika jopo hilo kama nchi, hasa kwa kuzingatia uhuru wake wa kujitawala na mivutano ya kidiplomasia baina yake na baadhi ya nchi zinazomshinikiza rais Kabila kuheshimu katiba ya Congo.

Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon ©REUTERS/Heinz-Peter Bader

Hata hivyo, rais huyo hajaweka wazi msimamo wowote wa kutaka kugombea urais kinyume na katiba licha ya kuwepo kwa hofu kubwa ya Upinzani unaomtuhumu kutaka kufanya marekebisho ya Katiba na kuendelea kubaki madarakani.

Hofu hiyo ilikolezwa na matamshi ya Katibu mkuu wa chama cha Kabila cha PPRD, Mova Sakani, ambaye tarehe 4 Juni chama hicho kimesherehekea miaka 45 ya kuzaliwa kwa rais Kabila, amesema kuwa mtu hawezi kustaafu akiwa na miaka 45 na kwamba raia wenyewe wanaweza kutoa maoni yao hata kwa njia ya kura ya maoni.

Hali ya kisiasa inaendelea kudorora nchini DRC kuelekea uchaguzi, huku kukiwepo na matukio ya mauaji Mashariki mwa nchi hiyo hususan maeneo ya Beni, Butembo na Lubero.