UTAFITI - TWAWEZA - TANZANIA

Watu 8 kati 10 wanapinga Bunge la Tanzania kutooneshwa moja kwa moja

Baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania
Baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania RFI

Watanzania walio wengi sawa na 79 hawakubaliani na maamuzi ya serikali ya kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge kupitia runinga na redio. 

Matangazo ya kibiashara

Wananchi wote wanaofikia asilimia 92 wanaamini kuwa ni muhimu vikao hivyo virushwe moja kwa moja.

Takwimu hizi zimetolewa na Twaweza kupitia muhtasari wa matokeo ya utafiti wake, ambapo muhtasari huo unahusisha takwimu zilizokusanywa na Sauti za Wananchi, Utafiti wa kwanza barani Afrika unaotumia simu za mkononi na wenye uwakilishi wa kitaifa.

Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa watu waliohojiwa elfu 1 mia nane na 15 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara huku upande wa Zanzibar ukiwa haujahusishwa kwenye utafiti huu uliofanyika kati ya tarehe 29 Machi na tarehe 12 Aprili 2016.

Miongoni mwa watanzania waliokua wakitazama na kusikiliza vipindi vya Bunge asilimia 42 walikuwa wakiangalia vikao vya Bunge vilivyokuwa vikirushwa moja kwa moja kupitia runinga na asilimia 60 walikuwa wakisikiliza vikao hivyo kupitia redio.

Kati ya hawa, asilimia 59 waliangalia vipindi vya Bunge kupitia runinga miezi miwili kabla ya utafiti huu kufanyika, na asilimia 57 walisikiliza vipindi vya Bunge kupitia redio.

Takwimu hizi zinaonyesha kuwa wananchi walikuwa wafuatiliaji wazuri wa vikao vya Bunge vilivyokuwa vikirushwa moja kwa moja, ambapo walieleza sababu zao walizosema za msingi.

Sababu hizo ni pamoja na asilimia 46 ya wananchi wanataka kuwafuatilia wabunge wao ili kuona kama wanawawakilisha ipasavyo, asilimia 44 wanasema ni haki yao kufahamu kile kinachoendelea bungeni, asilimia 29 wanaamini zaidi matangazo ya moja kwa moja kwa sababu wanawaona na kuwasikia wabunge kwa macho na masikio yao wenyewe

Walipoulizwa kuhusu matumizi ya fedha za umma kugharamia matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge, asilimia 80 ya wananchi wamesisitiza kuwa matangazo hayo yana umuhimu sambamba na huduma nyingine za jamii.

 

Kwenye utafiti huo, umeonesha kuwa wananchi walio wengi ambao ni sawa na asilimia 88 wanasema matangazo ya vikao vya Bunge yarushwe moja kwa moja bila kujali gharama, huku wengine wakiwa wanaunga mkono kwa kiwango kikubwa suala la kuruhusiwa kwa vyombo binafsi vya habari kurusha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge iwapo serikali imeshindwa kuyagharamaia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, anasema “suala la kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge la Tanzania limezua mjadala mzito miongoni mwa watanzania. Kupitia Sauti za Wananchi, tunaona wazi kabisa shauku kubwa ya wananchi ya kutaka kuwaona na kuwasikia wawakilishi wao bungeni kwa macho na masikio yao wenyewe. Je, serikali iko tayari kuyapokea matakwa ya watanzania walio wengi katika jambo hili? Ikibadilisha maamuzi yake na kurudisha matangazo haya itakua ishara nzuri ya nia yake ya kuimarisha uhusiano wa karibu zaidi kati ya wananchi na wabunge wao.” alisema.