DRC - USALAMA

Bunge: Serikali ianzishe uchunguzi mauaji ya Beni.

Wanajeshi wa Serikali wakiwa kwenye doria mjini Beni mashariki mwa DRC
Wanajeshi wa Serikali wakiwa kwenye doria mjini Beni mashariki mwa DRC UN Photo/Sylvain Liechti

Bunge la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo juma hili limehitimisha vikao vyake vya siri kuhusu hali ya usalama Mashariki mwa nchi hiyo hususan eneo la Beni, na kuitaka Serikali kuanzisha uchunguzi kuhusu mauaji yanayoendelea kushuhudiwa kwenye eneo hilo.

Matangazo ya kibiashara

Moja ya maazimio ya vikao hivyo ambavyo havikuoneshwa na runinga, ni pomoja na kuitaka Serikali kukomesha haraka iwezekanavyo mauaji ya Beni kwa kutumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama.

Aidha, kamati ya ulinzi na usalama ya Bunge inaomba pawepo na uchunguzi wa kitaifa na kimataifa kuwabaini wahusika wa mauaji hayo sawia na kuendelezwa kwa operesheni ya kuyatokomeza makundi ya waasi wa ADF, FDLR na makundi mengine, mashariki mwa nchi.

Sanjari na hayo, wabunge nchini humo wanaitaka serikali kuwatambua wakimbizi walioko kwenye makambi, pamoja na kufafanua asili yao kwa lengo la kuwarejesha makwao.

Wanajeshi wa Monusco wakiwa kwenye doria mjini Beni
Wanajeshi wa Monusco wakiwa kwenye doria mjini Beni UN Photo/Sylvain Liechti

Eneo la mashariki mwa Congo linakabiliwa na machafuko na mauaji kwa zaidi ya miongo miwili ambapo wilaya ya Beni imekumbwa na mauaji ya raia wake yanayotekelezwa na watu wasiojulikana tangu mwaka 2014, ambapo idadi ya waliouawa inakadiriwa kufikia watu zaidi ya elfu moja.

Mijadala ya Bunge ambalo wabunge walio wengi ni wa vyama vinavyomuunga mkono Rais Joseph Kabila, inaibua maswali kadhaa ikiwa ni pamoja na kufahamu ni kwa nini Bunge liihoji Serikali hivi sasa, baada ya mauaji kutekelezwa kwa kipindi kirefu?

Mwezi Mei, wabunge kutoka eneo la mashariki hasa katika jimbo la Kivu Kaskazini wamesusia vikao vya Bunge kushinikiza ukweli wa matukio ya Beni ubainishwe na kujadiliwa Bungeni.

Watoto wakionekana kwenye kambi ya wakimbizi Miriki walikokimbilia kukwepa mashambulizi ya kundi la FDLR mjini Beni
Watoto wakionekana kwenye kambi ya wakimbizi Miriki walikokimbilia kukwepa mashambulizi ya kundi la FDLR mjini Beni RFI / Sonia Rolley

Wachambuzi wa masuala ya Congo wanahoji ikiwa matakwa ya wabunge hao yatafikiwa ukizingatia chunguzi nyingine ambazo zimedaiwa kuendeshwa bila ya mafanikio au bila ya taarifa kamili za matokeo kama ilivyokuwa juma lililopita kwa ripoti ya operesheni “Likofi” ya Februari 2014 mjini Kinshasa, ambapo kwa mujibu wa mashirika ya kiraia, watu wasiopungua 50 wamepoteza maisha yao.

Mwaka uliopita, mashirika hayo na vyama vya upinzani yaliomba pawepo na uchunguzi wa kimataifa kufuatia kugunduliwa kwa kaburi la pamoja lenye miili ya watu zaidi ya mia nne katika kitongoji cha Maluku pembezoni mwa mji mkuu wa Kinshasa bila ya mafanikio yoyote.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Gavana wa Jimbo la Kivu Kaskazini, Julien Paluku, amechapisha waraka kwa wakuu wa wilaya zote husika jimboni humo kutaka kusitishwa kwa uzururaji wa watu wasiotambulika jimboni humo.

Suala la usalama mashariki mwa DRC linaendelea kuibua maswali na kuzorotesha mahusiano ya Congo na majirani zake wa mashariki wanaotuhumiwa kukodolea macho rasilimali zake na kusababisha makabiliano ya hapa na pale ya askari wa pande mbili za mipakani, tukio la mwisho likiwa la mauaji ya askari watatu wa Uganda Mei 22 mwaka huu.