MO IBRAHIM

Hakuna mshindi wa tuzo ya Mo Ibrahim mwaka 2015

Mwenyekiti wa kamati ya tuzo za Mo Ibrahim, Dr. Salim Ahmed Salim
Mwenyekiti wa kamati ya tuzo za Mo Ibrahim, Dr. Salim Ahmed Salim RFI

Taasisi ya mfuko wa Mo Ibrahim, Alhamisi, Juni 16, imetangaza kuwa hakuna mshindi wa tuzo ya kiongozi bora Afrika kwa mwaka 2015. 

Matangazo ya kibiashara

Tangazo hili limetolewa baada ya kufanyika kikao cha kamati huru inayosimamia tuzo ya Mo Ibrahim, inayoongozwa na mwenyekiti, Dr. Salim Ahmed Salim.

Akizungumza baada ya kutolewa kwa tangazo la kamati inayosimamia tuzo ya Ibrahim, mwenyekiti wa taasisi hiyo, Mo Ibrahim, amesema kuwa "bodi inaheshimu uamuzi wa kamati huru ya tuzo. Wakati ilipozinduliwa miaka 10 iliyopita, kwa makusudi kabisa tuliweka vigezo vya hali ya juu. Tunataka tuzo hii iwe mfano bora kwa viongozi wanaopewa ili kutengeneza mazingira mazuri ya utawala bora miongoni mwa jamii, sambamba na kuendelea kuwashawishi wakuu wa nchi kutawala vizuri bara la Afrika." alisema Mo.

Washindi wanaoweza kupewa tuzo hiyo ni wale waliowahi kuwa marais wa nchi za Afrika, ambao waliondoka madarakani miaka mitatu iliyopita, na walichaguliwa kidemokrasia na kutawala kwa mujibu wa katiba.

Taarifa ya kamati inayosimamia tuzo ya Ibrahim, tayari imeanza kupitia wakuu wa nchi ambao wanaweza kushinda tuzo hii kwa mwaka 2016.

Toka tuzo hii ilipozinduliwa mwaka 2006, tuzo ya Mo Ibrahim imeshakabidhiwa kwa marais wa zamani ambao ni Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohamba aliyeshinda mwaka 2014, Rais wa visiwa vya Cape Verde, Pedro Pires aliyeshinda mwaka 2011, Rais wa Botswana, Festus Mogae aliyeshinda mwaka 2008, Rais wa Msumbiji, Joaquim Chissano aliyeshinda mwaka 2007.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini marehemu, Nelson Mandela, yeye alipewa tuzo hii kwa heshima ya mchango wake kwa bara la Afrika mwaka 2007.