AFRIKA - MTOTO WA AFRIKA

Siku ya mtoto wa Afrika: Ni wajibu wetu kuwalinda watoto

Baadhi ya watoto wanaotumikishwa kama wanajeshi kwenye maeneo ya vita
Baadhi ya watoto wanaotumikishwa kama wanajeshi kwenye maeneo ya vita HRW

Bara la Afrika linaadhimisha siku ya mtoto wa Afrika, siku ambayo kilele chake ni tarehe 16 Juni kila mwaka, lengo likiwa ni kuikumbusha jamii na mataifa ya Afrika kuhusu umuhimu wa kulinda na kutetea haki za watoto.

Matangazo ya kibiashara

Kauli mbiu ya mwaka huu ni "vita na migogoro barani Afrika: Tulinde haki zote za watoto."

Siku hii inaadhimishwa wakati ambapo nchi nyingi za Afrika wakati huu zinakabiliwa na migogoro na vita za wenyewe kwa wenyewe, ambapo kwa sehemu kubwa wanaoathirika kwenye machafuko haya ni watoto.

Mkataba wa haki na hali za watoto kwa mara ya kwanza uliridhiwa na uliokuwa umoja wa Afrika OAU Julai 11 mwaka 1990 na kuanza kutekelezwa tarehe 29 November mwaka 1999, baada ya miaka 25 toka mkataba huo kuridhiwa ambapo nchi 47 za Afrika zilitia saini mkataba huu.

Nembo ya umoja wa Afrika, AU.
Nembo ya umoja wa Afrika, AU. www.au.int/

Nchini Tanzania tatizo la ndoa za utotoni, unyanyasaji wa kijinsia na ubakaji ni miongoni mwa masuala yanayoangaziwa kwenye maadhimisho ya mwaka huu, ambapo Serikali imeapa kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kuwalawiti na kuwabaka watoto wadogo.

Tatizo la ndoa za utotoni haliko tu nchini Tanzania lakini karibu kwenye nchi zote za ukanda wa Afrika Mashariki, kilio kikubwa cha mashirika ya kiraia kimekuwa ni ukatili na unyanyasaji wanaofanyiwa watoto.

Umoja wa Afrika unasema kuwa vita kwenye nchi za Sudani Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, DRC, makundi ya kijihadi kama ya Boko Haram nchini Nigeria, Niger na Cameroon, maelfu ya watoto wameathirika kutoka kwenye maeneo haya kutokana na machafuko yanayoendelea kushuhudiwa.

Umoja wa mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watoto milioni nne duniani, wanatumikishwa kwenye maeneo ya vita, suala ambalo ikiwa halitachukuliwa hatua kudhibiti wimbi la watoto kutekwa na kutumikishwa kwenye makundi ya waasi, basi miaka michache ijayo idadi hii itaongezeka maradufu.