MISRI

Kisanduku cha pili cha sauti chapatikana kutoka ndege ya Misri

Moja ya visanduku viwili vyeusi vya ndege ya shirika la ndege la EgyptAir chapatikana
Moja ya visanduku viwili vyeusi vya ndege ya shirika la ndege la EgyptAir chapatikana AFP/BEA

Wachunguzi wa ajali za ndege nchini Misri, wamefanikiwa kupata kisanduku kingine cha sauti kutoka kwenye ndege ya shirika la Misri “EgyptAir” iliyoanguka kwenye bahari ya Mediterrania mwezi mmoja uliopita.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa za kupatikana kwa kisanduku kingine cha sauti, zinakuja ikiwa siku moja tu imepita, toka maofisa hao, waripoti kufanikiwa kukipata kisanduku cha sauti kinachokaa kwenye eneo la bawa la mwisho wa ndege.

Wataalamu hao wanasema kuwa kisandukuj hicho cha sauti kimepatikana kwenye eneo moja na kile cha kwanza ambapo mtambo maalumu unaoweza kufika kwa sakafu ya bahari, ulifanikiwa kubaini eneo halisi yaliko mabaki yote ya ndege namba MS804.

Visanduku vyote viwili vilivyopatikana vinafahamika kama “black box” ama visanduku vyeusim na kupatikana kwake ni muhimu katika kusaidia uchunguzi wa unaoendelea kubaini sababu hasa za ndege hiyo aina ya Airbus A320 ipoteze mawasiliano kwenye rada na kuanguka May 19 na kuua watu wote 66 waliokuwemo.

Wachunguzi wa Misri na wale wa kimataifa wanasema kuwa ni mapema mno kueleza ni kitu gani hasa kiliipata ndege hiyo mpaka kuanguka ama ikiwa ni kweli lilikuwa shambulio la kigaidi kama linavyoripotiwa na baadhi ya wataalamu.

Ndege hiyo, ilipotea wakati ikiwa safarini kutokea jijini Paris, Ufaransa kuelekea Cairo Misri, ikiwa na abiria 66.

Wachunguzi wa Misri bado wanaendelea kufanya jithada kufanikisha kutoa nyaraka zilizokuwemo kwenye visanduku vyote viwili, ambapo kimoja hutumika kurekodi taarifa na mwenendo wa ndege na kingine hurekodi mawasiliano ya marubani wa ndege.