ERITREA-MSF

MSF yatoa msaada kwa wakimbizi wa Eritrea

Wakimbizi wa Eritrea wakiingia ndani ya basi na kupelekwa katika kambi ya Hitsats, kaskazini mwa Ethiopia.
Wakimbizi wa Eritrea wakiingia ndani ya basi na kupelekwa katika kambi ya Hitsats, kaskazini mwa Ethiopia. © UNHCR/K.GebreEgziabher

Shirika la Madaktari wasio na mipaka (MSF) limeanza kuwasaidia maelfu ya wakimbizi wa Eritrea walioko katika makambi kadhaa kaskazini mwa Ethiopia.

Matangazo ya kibiashara

Baadhi wako katika makambi hayo kwa miaka kadhaa, na maelfu wengine bado wanaendelea kuwasili kila mwezi, wakikimbia mateso wanayofanyiwa na serikali ya Asmara. Miongoni mwa wakimbizi hawa, baadhi hawakuweza kuingia Ulaya, lakini wamepata matatizo kutokana na barabara hatari wanayotumia kuelekea Sudan, Misri na Libya ili kujaribu kuingia Ulaya. MSF imeanzisha mpango wa kisaikolojia au kiakili, kuwasaidia wakimbizi ambao wanahitaji.

Wengi wao walivuka mpaka wakati wa usiku bila mizigo. Baadhi waliponea kutumiwa katika biashara ya binadamu iliyoandaliwa na watu waliokua wakiwasafirisha na ambao hawakua waaminifu kwao. Na wakati mwingine walishuhudia wemzao wakifariki kwa sababu mbalimbali, kama vile magonjwa, njaa na uchovu. Hakuna la ajabu, kuona kwamba hali ya kisaikolojia ya wakimbizi hawa wa Eritrea ni tete.

Lakini subira na elimu ni maneno muhimu ya kuwapa wale ambao wanahitaji kuhudumiwa. "Baadhi wana matatizo mengi na inachukua muda ili kupata imani yao kabla ya kuweza kuwaeleza ni msaada gani tunaotoa na kwa nini. Lakini hadi sasa zoezi hili linakwenda vizuri. Tunaeleza mchakato wetu katika makambi, katika jamii zinazoishi jirani ya makambi hayo, na kwa wale ambao wana matatizo halisi ya akili, tunatoa huduma katika mazingira ya wazi, lakini pia katika mazingira ya siri. Huko, tunafanya kazi kwa ushirikiano na wenzetu wataalamu wa matatizo ya akilikutoka Ethiopia, " Oliver Schultz, mkuu wa MSF nchini Ethiopia, amesema.

Wagonjwa wenye matatizo ya akili ndio wanaomba msaada wa kisaikolojia. Na mara nyingi, hii inafanyika kwa hatua. "Hii inaweza kuanza na tiba ya kikundi, kabla ya kuhamia kwenye vikao vya kila mmoja. Wakati mwingine, tunaandaa sherehe kwa watu wote, na watu kutoka jamii mbalimbali wanaweza tu kuhudhuria, kusikiliza na wakati mwingine kupeana mitazamo tofauti, " Olivier Schultz ameomngeza.

Msaada huu wa kisaikolojia, MSF inatoa kwa wakimbizi wa Eritrea, lakini pia kwa raia wa Ethiopia wanaowapokea wakimbizi hao.

■ Eritrea: kesi ya kitaifa ya watu 400 000 na wafungwa wa kisiasa

Jumanne, Juni 21, Tume ya ya Uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Eritrea itawasilisha ripoti yake kwa Baraza la Haki za Binadamu. Ripoti inayoinyooshea kidole cha lawama utawala wa Rais Issayas Afewerki. Ripoti hiyo inabaini kwamba viongozi wa Eritrea wana hatia ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, dhidi ya raia tangu mwaka 1991. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu 400,000 ni "watumwa" kwa sababu ya wanatumiwa kwa kazi za kijeshi kwa muda usiojulikana. Shutma ambazo Waziri wa Mambo ya Nje wa Eritrea, Osman Saleh, ametupilia mbali.