DRC-CAR-BEMBA-ICC

Jean-Pierre Bemba ahukumiwa kifungo cha miaka 18 jela

Jean-Pierre Bemba, akiwa kwenye mahakama ya ICC mwezi Machi mwaka 2016.
Jean-Pierre Bemba, akiwa kwenye mahakama ya ICC mwezi Machi mwaka 2016. REUTERS/JERRY LAMPEN/Pool

Majaji wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC, yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi, wamemuhukumu kifungo cha miaka 18 jela, aliyewahi kuwa makamu wa rais kwenye Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

Matangazo ya kibiashara

Hukumu dhidi ya Bemba inatolewa ikiwa ni miezi michache imepita toka mahakama hiyo, imkute na hatia ya makosa ya uhalifu wa kivita na vitendo vya ubakaji vilivyotekelezwa na askari wake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mwezi Machi mwaka huu mahakama ya ICC baada ya kusikiliza pande zote kwenye kesi husika, na baada ya Jean-Pierre Bemba mwenyewe kuomba radhi kutokana na yale yaliyotokea wakati akiwa kiongozi, bado ilimkuta na hatia.

Jean-Pierre Bemba Gombo alikamatwa na maofisa usalama wa Ubelgiji Mei 24 mwaka 2008, baada ya kutolewa kwa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwake na alijisalimisha kwenye mahakama hiyo, Juni 3 mwaka 2008.

Juni 15 mwaka 2009 majaji wa mahakama ya ICC walithibitisha mashtaka dhidi yake, ambapo kesi yake ilianza kusikilizwa November 22 mwaka 2010 na taarifa za kufungwa kwa kesi yake zilisomwa kati ya November 12 na 13 mwaka 2014.

Jean-Pierre Bemba.
Jean-Pierre Bemba. REUTERS/Michael Kooren/Files

Awali waendesha mashataka wa mahakam hiyo, waliiomba mahakama imuhukumu kifungo cha miaka isiyopungua 30 jela, kutokana na makosa yenyewe aliyokutwa nayo na hatia.

Licha ya upande wa utetezi kudai kuwa mteja wao hakuhusika kwa vyovyote vile kutekeleza uhalifu dhidi ya binadamu, majaji wa mahakama hiyom walijiridhisha pasipo na shaka kuwa Bemba alishiriki kwenye kuamrisha askari wake kutekeleza uhalifu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati, kwa muda mrefu wametaka kukamatwa kwa wahusika wakuu wa machafuko yaliyoshuhidwa na sio kumshikilia Bemba peke yake kwa kile wanachoamini kuwa uhalifu ule haukutekelezwa na yeye peke yake.

Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanaona kuwa licha ya kuwa hukumu hii inaweza isiwe tiba ya wahanga wa vitendo vya ubakaji na udhalilishaji, angalau imetenda haki kwa mtuhumiwa ambaye yeye mwenyewe aliomba radhi mahakamani na kutaka apunguziwe adhabu.

Bemba alishtakiwa kwa makosa yaliyotekelezwa kati ya October 2002 na Machi 2003, kwa kumuunga mkono rais Ange-Felix Patasse aliyekuwa akikabiliwa na jaribio la kupinduliwa na Jenerali Francois Bozize ambaye baadae alikuwa rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.