DRC-SIASA-KATUMBI

Moise Katumbi, ahukumiwa kifungo cha miaka 3 jela

Mwanasiasa wa upinzani Moise Katumbi akiasindikizwa na wafuasi wake mahakamani, mjini Lubumbashi, Mei 11, 2016.
Mwanasiasa wa upinzani Moise Katumbi akiasindikizwa na wafuasi wake mahakamani, mjini Lubumbashi, Mei 11, 2016. © REUTERS/Kenny Katombe

Mahakama moja mjini Kamalondo, Lubumbashi, imemuhukumu kifungo cha miaka 3 jela, aliyekuwa gavana wa jimbo la Katanga na mgombea urais kupitia muungano wa vyama vya upinzani, Moise Katumbi Chapwe.

Matangazo ya kibiashara

Katumbi alishtakiwa mahakamani kwa tuhuma za kumdhulumu nyumba raia mmoja wa Ugiriki, Alexander Stoupis, tuhuma ambazo mara zote, Katumbi amekuwa akikanusha.

Hukumu hii ambayo imetolewa bila ya Katumbi mwenyewe kuwepo mahakamani kutokana na kuwa nje ya nchi akiendelea kupatiwa matibabu, imeamsha hisia kali miongoni mwa wafuasi wake na vyama vya upinzani.

Tayari aliyekuwa spika wa Bunge la Katanga na mmoja wa wanachama wa muungano wa G7, Kyungu Wakumwanza, amekosoa hukumu hiyo akisema ni ya uonevu na inayolenga kummaliza kisiasa, Katumbi.

Mbali na kuhukumiwa kifungo gerezani, mahakama pia imemtaka alipe faini ya kiasi cha dola za Marekani, milioni moja kama fidia kutokana na dhuluma aliyoifanya.