ICC-DRC-BEMBA

Wafuasi wa Jean-Pierre Bemba walaani uamuzi wa kidhalimu

Umati wa wafuasi wa Jean-Pierre Bemba walikuwa wamekusanyika katika makao makuu ya chama cha MLC katika mji wa Kinshasa kufuata kufuata moja kwa moja uamuzi kwenye televisheni uamuzi wa ICC dhidi ya Jean-Pierre Bemba, tarehe 21 Juni 2016.
Umati wa wafuasi wa Jean-Pierre Bemba walikuwa wamekusanyika katika makao makuu ya chama cha MLC katika mji wa Kinshasa kufuata kufuata moja kwa moja uamuzi kwenye televisheni uamuzi wa ICC dhidi ya Jean-Pierre Bemba, tarehe 21 Juni 2016. RFI/Sonia Rolley

Majaji wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya ICC, yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi, wamemuhukumu kifungo cha miaka 18 jela, aliyewahi kuwa Makamu wa rais kwenye Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Matangazo ya kibiashara

Hukumu dhidi ya Bemba inatolewa ikiwa ni miezi michache imepita toka mahakama hiyo, imkute na hatia ya makosa ya uhalifu wa kivita na vitendo vya ubakaji vilivyotekelezwa na askari wake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mwezi Machi mwaka huu mahakama ya ICC baada ya kusikiliza pande zote kwenye kesi husika, na baada ya Jean-Pierre Bemba mwenyewe kuomba radhi kutokana na yale yaliyotokea wakati akiwa kiongozi, bado ilimkuta na hatia.

Jean-Pierre Bemba Gombo alikamatwa na maofisa usalama wa Ubelgiji Mei 24 mwaka 2008, baada ya kutolewa kwa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwake na alijisalimisha kwenye mahakama hiyo, Juni 3 mwaka 2008.

Juni 15 mwaka 2009 majaji wa mahakama ya ICC walithibitisha mashtaka dhidi yake, ambapo kesi yake ilianza kusikilizwa November 22 mwaka 2010 na taarifa za kufungwa kwa kesi yake zilisomwa kati ya November 12 na 13 mwaka 2014.

Awali waendesha mashataka wa mahakam hiyo, waliiomba mahakama imuhukumu kifungo cha miaka isiyopungua 30 jela, kutokana na makosa yenyewe aliyokutwa nayo na hatia.

Licha ya upande wa utetezi kudai kuwa mteja wao hakuhusika kwa vyovyote vile kutekeleza uhalifu dhidi ya binadamu, majaji wa mahakama hiyom walijiridhisha pasipo na shaka kuwa Bemba alishiriki kwenye kuamrisha askari wake kutekeleza uhalifu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati, kwa muda mrefu wametaka kukamatwa kwa wahusika wakuu wa machafuko yaliyoshuhidwa na sio kumshikilia Bemba peke yake kwa kile wanachoamini kuwa uhalifu ule haukutekelezwa na yeye peke yake.

■Raia wa Congo wagawanyika kuhusu hukumu dhidi ya Bemba

Katika mji wa Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wengi walipokea kwa shingo upande uamuzi huo wa majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu Jumanne hii wakisema hawaelewi uzito wa hukumu. Hata hivyo, wengine ameona kama uamuzi huo wa ICC ni mfano kwa viongozi ambao wana dhamira au nia ya kufanya ukatili alioufanya Jean- Pierre Bemba na wapiganaji wake.

Mabango ya kumuunga mkono Jean-Pierre Bemba kwenye makao makuu ya cchama cha MLC.
Mabango ya kumuunga mkono Jean-Pierre Bemba kwenye makao makuu ya cchama cha MLC. RFI/Sonia Rolley