DRC

Watu 75 wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji na ubakaji DRC

RFI

Mamlaka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, zinawashikilia watu zaidi ya 75 kwa tuhuma kuwa ni wapiganaji wanaosakwa kwa vitendo vya mauaji na ubakaji, kwenye jimbo la Kivu Kusini.

Matangazo ya kibiashara

Mtandao wa kundi hili la wapiganaji, unatuhumiwa kuwalenga wasichana wadogo, wanaowahusisha na imani za kishirikina kuwa wanawapa ulinzi.

Miongoni mwa watu wanaoshikiliwa na vyombo vya usalama, ni pamoja na anayetuhumiwa kuwa ni kiongozi wao, Frederic Batumike, ambaye ni naibu gavana.

Haya yanaripotiwa wakati huu ambapo nchi ya DRC inaendelea kuponya vidonda vya machafuko yanayoendelea kushuhudiwa kwenye eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Waziri wa sheria wa DRC, Alexis Thambwe Mwamba, amesema kuwa Batumike na watu wengine 74 wanaodaiwa kuwa ni wapiganaji wake, walikamatwa juma lililopita, kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya kujirudia ya vitendo vya ubakaji kwa imani za kishirika.

"Wapiganaji wanaomfanyia kazi wamekuwa wakiajiri watu wanaowashauri kuwabaka wasichana wadogo, kwa imani kuwa kufanya hivyo kutawapa ulinzi." alisema waziri Thambwe.

Waziri huyo wa sheria ameongeza kuwa, Batumike alikuwa anatuhumiwa pia kuagiza mauaji ya injinia raia wa Ujerumani, Walter Muller na mwanaharakati wa haki za binadamu nchini DRC, Evariste Kasali.