MAREKANI-AFRIKA

Mke wa Rais Obama ziarani barani Afrika

REUTERS/Jonathan Ernst

Mke wa rais wa Marekani, Michelle Obama, anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi barani Afrika, Jumapili hii, akiambatana na watoto wake, Sasha na Malia, ziara ambayo ni sehemu ya juhudi zake za kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike. 

Matangazo ya kibiashara

Ziara hii ya siku sita barani Afrika, itashuhudia mke wa rais Obama, akisafiri kwenye nchi za Morocco na Liberia, ambapo pia atasafiri hadi Hispania.

Ziara ya Michelle Obama imebeba ujumbe wa "Waache wasichana wasome", ilizinduliwa na Serikali ya Marekani kupitia rais Barack Obama na mkewe mwenyewe mwaka 2015.

Mradi huu ni sehemu ya Serikali ya Marekani katika juhudi zake za kueneza elimu na kuondoa vikwazo ambavyo vinawazuia zaidi ya wasichana milioni 62 duniani kutokwenda shule.

Kwenye ziara hiyo, Michelle atasindikizwa na muigizaji, Meryl Streep na Freida Pinto nchini Morocco, ambako watazungumza na wasichana wadogo kuhusu changamoto zinazowakabili kupata elimu, ilisema taarifa ya ofisi ya mke wa rais.

Akiwa nchini Liberia, atatembelea kituo cha Marekani cha wafanyakazi wa Marekani wanaojitolea, pamoja na shule moja ya wasichana akiambatana na rais wa Liberia, Ellen Johansson Sirleaf, mwanamke wa kwanza Rais aliyechaguliwa kidemokrasia na mshindi wa tuzo la Nobel.

Nia ya Michelle Obama kuwasaidia wasichana kupata elimu, ilizidi baadaya tukio la kutekwa nyara kwa wasichana zaidi ya 200 wa Chibok kaskazini mwa Nigeria, mwezi Aprili mwaka 2014, ambapo aliandika kwenye mtandao wake #BringBackOurGirls.