SOMALIA

Mlipuko mkubwa waripotiwa mjini Mogadishu, hoteli yalengwa

MOja ya gari lililoharibiwa na mlipuko wa bomu mjini Mogadishu hivi karibuni.
MOja ya gari lililoharibiwa na mlipuko wa bomu mjini Mogadishu hivi karibuni. Reuters/Feisal Omar

Kumeshuhudiwa mlipuko mkubwa kwenye hoteli moja mjini Mogadishu, Somalia, ambapo ulifuatiwa na makabiliano ya risasi kati ya vikosi vya Serikali na wapiganaji wanaodaiwa kuwa ni wa Al-Shabab.  

Matangazo ya kibiashara

Waandishi wa habari walioko mjini Mogadishu wanasema kuwa, makabiliano ya risasi bado yanaendelea ndani ya hoteli ya Naso Hablod hotel iliyoko maili moja tu na uwanja wa ndege wa Mogadishu.

Maofisa usalama mjini Mogadishu wamethibitisha makabiliano ya risasi kuwa yanaendelea bila ya kutoa taarifa nyingine zaidi.

Mwanahabari wa shirika la AFP aliyeko mjini Mogadishu, amesema kuwa, awali kulianza kushuhudiwa milipuko ya mabomu ya kujitoa muhanga kabla ya hoteli hiyo kuvamiwa na watu wenye silaha.

Shambulio hili linajiri ikiwa ni wiki tatu tu zimepita, toka kutekelezwa kwa shambulio jingine kama hilo kwenye hoteli ya Ambassador, ambapo watu zaidi ya 10 waliuawa, wakati bomu la kutegwa kwenye gari lilipolipuka.

Wapiganaji wenye silaha toka kundi la Al-Shabab walikabiliana na vikosi vya Serikali kwa zaidi ya saa 12.

Hoteli ya Naasa Hablood iliyoko kusini mwa mji wa Mogadishu, ni nadra kutumiwa na wanasiasa na wabunge wa Serikali pamoja na wageni wanaotembelea nchi hiyo.