Watu 11 wauawa katika shambulizi la Al Shabab mjini Mogadishu
Imechapishwa:
Takriban watu 11 wameuawa jana Jumamosi katika shambulizi kwenye hoteli ya mjini Mogadishu nchini Somalia ambalo linadaiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Al Shabaab.
Shambulizi hilo ambalo ni la karibuni katika mfululizo wa mashambulizi yanayotekelezwa na kundi la Al Shabab kulenga hoteli na migahawa, lilianza wakati mshambuliaji wa kujitoa mhanga alipolipua bomu lililokuwa limetegwa garini nje ya jengo la hoteli.
Watu wenye silaha walivamia hoteli iitwayo Naasa Hablood na milio ya risasi ilisikika kwa saa kadhaa, mashahidi wamesema, kabla ya mamlaka kutangaza mashambulizi kumalizika.
Vikosi maalum vya usalama vimekomesha shambulizi hilo baada ya kuwaua washambuliaji watatu ndani ya hoteli.
Msemaji wa wizara ya usalama Abdi Kamil Shukri, amewaambia waandishi wa habari kuwa raia kumi na mmoja, wawili kati yao madaktari, wameuawa katika shambulio hilo.