DRC-KABILA

Maaskofu DRC, wataka uchaguzi ufanyike kwa wakati

Kushoto ni Kadinali Laurent Monsengwo Pasinya, ambaye baraza la maaskofu nchini humo Jumatatu ya wiki hii, wamemtaka Rais Kabila aondoke madarakani kwa amani.
Kushoto ni Kadinali Laurent Monsengwo Pasinya, ambaye baraza la maaskofu nchini humo Jumatatu ya wiki hii, wamemtaka Rais Kabila aondoke madarakani kwa amani. RFI

Kundi lenye ushawishi la maaskofu wa kanisa katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, wametoa wito wa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo kufanyika kama ulivyopangwa mwaka huu na kumtaka rais Josephu Kabila, kuondoka madarakani baada ya kutamatika kwa muhula wake wa pili.

Matangazo ya kibiashara

Rais Kabila ambaye amekuwa madarakani toka mwaka 2001, anatakiwa kuacha ofisi yake mwezi December mwaka huu. Lakini mwezi Mei mwaka huu, mahakama ya katiba nchini humo ilisema anaweza kubaki madarakani ikiwa uchaguzi mkuu wa rais hautafanyika ndani ya muda, huku upinzani ukimtuhumu kwa kutaka kuendelea kusalia madarakani kwa nguvu.

"Ni muhimu sana ikiwa tutaheshimu katiba", hasa linapokuja suala la "mihula ya rais wa Jamhuri kukaa madarakani," alisema mchungaji Leonard Santedi, katibu mkuu wa baraza la maaskofu, kwenye mkutano na wanahabari mjini Kinshasa.

Santedi amewataka wanasiasa nchini humo kuwa na utamaduni wa kukubali kuondoka madarakani na kubadilishana madaraka kwa amani kama msingi wa ukomavu wa demokrasia.

"Kuzuia mchakato wa uchaguzi kunatengeneza hofu, ambayo huenda ikasababisha kuzuka kwa machafuko kwenye nchi," alisema Santedi ambaye aliongeza kuwa "huu ni wajibu wa watawala wa kisiasa."

Joseph Kabila, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Februari 3, 2015.
Joseph Kabila, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Februari 3, 2015. © AFP PHOTO / CARL DE SOUZA

Kwenye ujumbe wao uliotolewa baada ya kumalizika kwa kikao chao cha 53 cha kila mwaka, maaskofu hao wamegusia kuhusu uvunjifu wa haki za binadamu unaoendelea kufanywa nchini humo, na hasa kwenye eneo la mashariki mwa nchi ya DRC ambako kuna mapigano baina ya makundi ya waasi.

Mkutano huu umefanyika wakati ambapo inaonekana kuwa Rais Kabila huenda akakaa madarakani kwa muhula wa tatu, lakini upinzani umeonya dhidi ya hatua hiyo na kwamba hawatavumilia kumuona akikaa madarakani zaidi ya December 19 wakati muhula wake wa pili utakapofika ukomo, na kwamba kuendelea kukaa madarakani baada ya muda huo ni sawa na kuifanyia mapinduzi katiba ya nchi.

Ijumaa ya wiki ilipita, Rais Kabila alisema Serikali yake itaandaa uchaguzi bila ya kuweka wazi ikiwa utafanyika ndani ya muda uliopangwa.