Watoto zaidi ya milioni 69 duniani wako hatarini kufariki
Imechapishwa:
Shirika la umoja wa Mataifa linalohusika na watoto duniani, UNICEF, limeitaka dunia kujielekeza zaidi katika kuwasaidia watoto masikini ili kuendelea kujenga maendeleo bora ya afya zao na elimu kama ilivyofanyika katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.
Kwenye ripoti yake iliyopewa jina la "State of the World's Children" yaani hali ya watoto duniani, imeeleza kupigwa kwa hatua ya kuzuia vifo vya watoto kwa asilimia 53 toka mwaka 1990, ikiwa ni hatua kubwa kupigwa wakati huu dunia ikikabiliwa na umasikini.
Lakini bila ya kuwa na mtazamo mmoja kuhusu watoto walio hatarini, ripoti hiyo imeonya kuwa, zaidi ya watoto milioni 69 walio na umri wa chini ya miaka 5 watakufa kutokana na maradhi sababu zinazoweza kuzuilika huku watoto milioni 167 wataathirika na umasikini katika kipindi cha miaka 15 ijayo.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, bila ya kutokea kwa mabadiliko yoyote kwa kipindi kirefu, watoto wanaokadiriwa kufikia milioni 750 wanawake na wasichana watakuwa wameolewa ifikapo mwaka 2030, mwaka ambao umoja wa Mataifa ulitenga kuwa siku ambayo malengo ya kuwa na dunia yenye maendele yamefikiwa.
Ripoti imeonesha kuwa hatua zilizopigwa sasa zimewalenga watoto ambao wanafikika kwa urahisi au upatikanaji wa tiba na chakula ni rahisi, alisema Justin Forsyth.
Forsyth ameongeza kuwa matokeo yanaonesha kuwa kama hatutawafikia watoto ambao ni waathirika wakubwa wa umasikini, basi malengi haya yanaweza yasifikiwe hivi karibuni.
Watoto walio masikini na wanaokabiliwa na utapia mlo hufa, ikiwa ni mara mbili zaidi kabla hawajafika umri wa miaka mitano, ukilinganisha na watoto walioko kwenye nchi zilizoendelea, ilisema ripoti ya UNICEF.
Ripoti imeongeza kuwa wasichana kutoka nchi masikini zaidi duniani wako hatarini zaidi kuolewa wakiwa watoto ukilinganisha na watoto wanaotoka kwenye familia zinazojiweza.