SUDANI KUSINI-USALAMA

Watu wasiopungua 40 wauawa Sudan Kusini

Wanajeshi wa Sudani Kusini katika uwanja wa ndege wa Bor, Kilomita 200 kaskazini mwa Juba.
Wanajeshi wa Sudani Kusini katika uwanja wa ndege wa Bor, Kilomita 200 kaskazini mwa Juba. REUTERS/George Philipas

Serikali ya Sudan Kusini imetangaza kuwa watu wasiopungua 40 wameuawa katika mapigano ya yaliyotokea hivi karibuni katika mji wa Wau na kubaini kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka.

Matangazo ya kibiashara

Tume ya umoja wa mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, imeweka nyenzo maalumu za usalama kuzunguka kambi yake iliyoko kwenye mji wa Wau, kufuatia kuzuka kwa mapigano kati ya wapiganaji wenye silaha na wanajeshi wa Serikali, SPLA.

Kwenye taarifa iliyotolewa na UNMISS, imesema kuwa inaendelea kutoa ulinzi kwa zaidi ya raia elfu 1, ambao wamenaswa kwenye mapigano yaliyoanza mwishoni mwa juma lilillopita.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa baada ya kufikiria kwa kina, iliamua kufungua milango yake siku ya Jumapili na kuruhusu mamia ya raia kuingia kwenye kambi yake, wakikimbia mapigano hayo.

Waziri wa Habari Michael Makuei, amesema kuwa maiti za raia 39 zimepatikana ikiwa ni pamoja na maiti nne za askari polisi.

Katika taarifa iliyotolewa na wakuu wa jimbo la Wau, baada ya kikao cha baraza la usalama la mji huo toka kulipozuka mapigano hayo Jumamosi ya wiki iliyopita, mkuu wa polisi kwenye mji huo, Chol Thuc amesema hali imeanza kurejea kama kawaida.

Msemaji wa jeshi la Sudan Kuisni alisema kuwa vikosi vyake vilipigana na makundi yaliyokuwa yamejihami pamoja na wale waliowataja kuwa wapiganaji wa makabila.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameonya kuhusu kuendelea kushuhudiwa kwa mapigano kwenye mji huo, ambapo maelfu ya raia wameendelea kuyakimbia makazi yao kwa hofu ya kiusalama.

Mashirika hayo yanautaka umoja wa Mataifa kuingilia kati hali hiyo, kwa kuvisaidia vikosi vya Serikali kukabiliana na makundi ya wapiganaji wenye silaha ambao wameendelea kutekeleza mashambulizi ya kushtukiza kwenye maeneo mengi ya nchi.